- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Kuzaliwa kwa Uongofu: Nuru Inayoondoa Giza Lililopo
(Imetafsiriwa)
Gazeti la Al-Rayah – Toleo 563 - 03/09/2025 M
Na: Ustadh Atiyah al-Jabareen – Ardhi Iliyobarikiwa – Palestina
Sayari ya Dunia, na hasa Bara Arabu, lilikuwa likiishi katika giza kuu lililofanya maisha ya binadamu yafanane na kuzimu. Kulikuwa na giza katika nyanja za itikadi, siasa, uchumi, mahusiano ya kijamii, na nyanja zote za maisha. Vita viliwasaga watu bila sababu, wenye nguvu walikuwepo huku wanyonge wakipotea na kutokuwepo, dhulma ilitanda maeneo yote, na utumwa ulifikia viwango vyake vya chini kabisa na vya udhalilishaji kabisa.
Hali hii ilibidi kutoweka na kufutiliwa mbali, na nuru ilibidi kuchomoza tena ili kumregesha ubinadamu kwa mwanadamu, na kuifanya haki na heshima kuwa msingi wa maisha ya mwanadamu, ambayo yalikuwa yamezama kwenye kina kirefu cha uwepo. Katikati ya giza hili, miale za nuru ilianza kutoboa, na kutuma miale ya matumaini kwa maisha mapya yaliyosimikwa juu ya utumwa wa kweli kwa Muumba wa uwepo, na kuishi kwa unyofu chini ya mifumo inayoleta furaha kwa mwanadamu na kumruhusu kuishi katika hali bora na ya juu zaidi.
Nuru hii ilianza kumulika ulimwengu mkubwa mnamo tarehe 12 Rabi ul-Awwal katika Mwaka wa Ndovu, kwani siku hiyo ilizuka nuru iliyomulika Mashariki na Magharibi ya Ardhi, kwa kuzaliwa Muhammad (saw). Nuru hii ilienea na kung’aa zaidi wakati Dunia ilipounganishwa na mbingu kwa kuchaguliwa kwake (saw) kama Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwa wanadamu wote.
Mtume (saw) alibeba mwenge wa nuru hii na akatembea nayo ili kuliondoa giza lote la Ardhi. Yeye (saw) aliteremsha kwa watu aqida (itikadi) na utumwa wa kweli ambao unakinaisha akili ya mwanadamu, uliomo ndani ya Iman kwa Mwenyezi Mungu (swt) Pekee, kumwabudu Yeye, na kumtukuza Yeye pekee. Yeye (saw) aliwanyanyua wale walioamini pamoja naye (saw), kutoka kwenye kina cha utumwa wa upotovu hadi kwenye kilele cha utumwa sahihi na safi, Dini sahihi. Yeye (saw) alibeba kwa watu mifumo ya maisha inayojumuisha nyanja zote na mahusiano ya uwepo wa mwanadamu, mifumo inayoafikiana na umbile la mwanadamu, na kumletea furaha ya milele na utulivu wa hali ya juu.
Miale ya nuru hii ilikamilishwa ili kulifuta giza wakati Dini hii na fikra hii ilipotoka kwenye nafasi ya udhaifu, na kwenda kwenye nafasi ya urithi na uwezeshaji kupitia nusrah (msaada wa kijeshi) wa watu wa Madina kwa Da’wah ya Mtume (saw), baada ya yeye (saw) kuomba nusra yao kama watu wenye uwezo na ulinzi. Nusrah hii ilisababisha kuanzishwa kwa chombo cha kwanza cha Kiislamu, dola kuu ya Kiislamu ya kilimwengu. Uislamu sasa ulitabikishwa kivitendo uwanjani ndani ya dola iliyobeba mwenge wa nuru yake kwa wanadamu wote, ili kuondoa giza la ukafiri na udhalimu.
Hivyo basi, kwa kuzaliwa Mtume (saw), utume wake, na ushindi wake, kulikuja kuzuka na kung’ara kwa nuru kuu, kuondoa dhulma na giza, na kumalizika kwa aina zote za upotofu katika aqida, ibada, na sheria. Hii pia ilikuwa ni mwanga na mfano kwetu wakati wowote giza linaporudi Duniani kama ilivyo leo. Kwa hiyo, nuru iko mikononi mwetu, na ni lazima tushikamane nayo kwa dhamira, tuibebe, na kuiregesha mkondo wake wa kwanza wa mapambano na makabiliano dhidi ya kila aina ya dhulma, giza, mkengeuko, na ufisadi, hadi nuru hii ipewe ushindi mpya, kuvikwa taji kwa kusimamishwa tena chombo na dola ya haki na uadilifu. Dola hii itaregesha Duniani nuru ambayo imefifia na kutoweka, kubadilisha hali kutoka kwenye kina cha giza hadi kwenye nuru, rehema, utulivu na uadilifu.
Hakika kuzaliwa kwa Mtume (saw), utume wake, na ushindi wake wa kusimamisha Dini, vilikuwa ni miale ya nuru kubwa iliyoimulika Dunia. Kwa hakika ni faradhi juu yetu kurudisha nuru hii duniani kwa mara nyengine tena kwa kurudisha mbebaji mwenge wake na muenezaji muangaza - Khilafah.