Ijumaa, 21 Safar 1447 | 2025/08/15
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Vita vya Sudan Vilivyosahauliwa: Janga kwa Ummah

"Hofu inayotokea nchini Sudan haina kikomo."
Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Turk

(Imetafsiriwa)

Sudan inavuja damu. Na ulimwengu hauelewi kabisa. Sasa ikiingia katika mwaka wake wa tatu mbaya, vita vya kikatili kati ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF), vinavyoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), vinavyoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti), vimeiingiza nchi katika machafuko na kuibua moja ya maafa ya kutisha zaidi ya kibinadamu ya zama zetu. Hata hivyo, licha ya ukubwa wa uharibifu na mateso, vita vya Sudan vinapuuzwa, kusahauliwa—vimenyamazishwa na kutojali kwa ulimwenguni.

Mapambano haya ya madaraka yamegharimu maisha ya takriban raia 150,000 tangu Aprili 2023 – ingawa mashirika ya misaada yanaamini kuwa idadi halisi ni kubwa zaidi. Hawa si wanajeshi kwenye medani za vita, bali wanawake, watoto na wazee waliouawa bila huruma majumbani mwao, misikitini, sokoni na kwenye kambi za muda (Chanzo: BBC).

Mauaji ya Al-Nahud, ambapo zaidi ya raia 300—ikiwemo watoto 21—waliuawa na wapiganaji wa RSF, ni moja tu ya ukatili mwingi. Miji yote imeteketezwa moto. Makaburi ya watu wengi yanachimbwa kwa haraka. Familia nzima zimepotea. Kinachotokea Sudan sio vita tu - ni maangamizi ya kimpangilio.

Wanawake na wasichana, kama kawaida katika vita, ni miongoni mwa wahasiriwa wanaodhulumiwa zaidi. Pande zote mbili zimetumia unyanyasaji wa kijinsia kama chombo cha ugaidi na udhibiti. Wasichana wa umri wa miaka 9 wametekwa nyara, kubakwa katika makundi, na kurudishwa wakiwa wameharibiwa kimwili—ikiwa kamwe watarudishwa. Walionusurika wanazungumza juu ya ubakaji wa hadharani uliokusudiwa kudhalilisha jamii na unyanyasaji mkubwa wa kingono katika kambi za watu waliohamishwa.

Wafanyikazi wa matibabu wanaripoti kuwatibu manusura wasioweza kufikia usaidizi wa kisaikolojia au haki. Wengi hukaa kimya, wakiogopa aibu au ulipizwaji kisasi. (Chanzo: Human Rights Watch, OHCHR)

Zaidi ya watu milioni 14 wamelazimika kuyahama makaazi yao—na kufanya hili kuwa janga kubwa zaidi la watu kuhama makwao duniani. Zaidi ya nusu ya raia milioni 50 wa Sudan wanakabiliwa na njaa. Kulingana na Mpango wa Chakula Duniani, njaa imeshika kasi katika majimbo 10, ikiwa ni pamoja na kambi ya Zamzam, ambayo ni makaazi ya watu 400,000 waliokimbia makaazi yao (Chanzo: WFP).

Chakula na maji ni haba. Si kwa sababu ya majanga ya kimaumbile—bali ya kubuni. Pande zote mbili zimetumia njaa kama silaha kwa kuzuia misaada ya kibinadamu, kukamata mahitaji yanayoletwa, na kunyima ufikiaji wa mahitaji ya kimsingi. Njaa inatumiwa kuadhibu watu wote.

Katika kambi za wakimbizi, watoto hula majani. Kina mama hukaa siku nyingi bila chakula kulisha watoto wao. Magonjwa yatokanayo na maji, malaria, na kipindupindu yameenea kwa kasi. Mifumo ya afya imeporomoka. UNICEF inaelezea hali hiyo kama mzozo wa sura nyingi, unaoharibu kila nyanja ya maisha—afya, usafi wa mazingira, elimu na usalama (Chanzo: WHO).

Ripoti nyingi zimeibuka kuhusu wafungwa wa kisiasa kuteswa, raia kutekwa nyara na watoto waliosajiliwa kwa nguvu kupigana. Wafanyikazi wa misaada ya kibinadamu pia wamekuwa wakilengwa—kuuawa, kutekwa nyara, au kunyimwa uwezo wa kuwafikia wale wanaohitaji. Hospitali zimeporwa na kugeuzwa kuwa viwanja vya vita. Shule zinapigwa mabomu. Hakuna mahali salama palipobakia (Chanzo: OHCHR).

Hata hivyo vyombo vya habari ni nadra sana kutaja jina la Sudan. Vita hivyo vinasifiwa kuwa visivyoonekana, kusahaulika, au kuachwa tu kutoka kwa vichwa vya habari kabisa. Tofauti na Ukraine au Gaza, hakuna uidhinishaji wa watu mashuhuri, hakuna maandamano makubwa, hakuna uharaka wa kisiasa.

Kimya cha Sudan sio wa bahati mbaya. Utajiri wake katika dhahabu, mafuta, urani, na ardhi yenye rutuba huifanya kuwa zawadi ya kimkakati ya kijiografia. Dola kama vile UAE, Saudi Arabia, Misri, Marekani, Uingereza, na Urusi zote zina hisa katika hatima ya Sudan. Nchi imekuwa bodi ya chess kwa maslahi ya nje.

Vita vya Sudan si ajali ya historia. Ni urithi wa ukoloni, mipaka yenye kugawanya, na tawala za dikteta za kisekula zilizoimarishwa na walinzi wa kigeni. Sudan, mithili ya sehemu kubwa ya ulimwengu wa Kiislamu, ilichongwa na kudhibitiwa na dola za kibeberu. Ilinyimwa uhuru wa kweli, uongozi wake ulifisidiwa, na watu wake wakapigana wao kwa wao.

Masuluhisho ya kidemokrasia yanayokuzwa na nchi za Magharibi ni sehemu ya tatizo. Mifumo hii – iliyoundwa kutumikia maslahi ya kipote cha wachache – imefeli Sudan, kama ilivyofeli Iraq, Libya, na Afghanistan.

Kuna njia moja tu inayotoa suluhisho la kweli, la kudumu kwa Sudan na Ummah mzima. Njia hiyo ni kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume.

Khilafah itawaunganisha Waislamu katika jamii na makabila tofauti, itaondoa ushawishi wa kigeni, itasambaza rasilimali kwa uadilifu, itaweka uwajibikaji, na kudhamini utu na usalama kwa wote. Historia inakumbuka jinsi utawala wa Khilafah chini ya Umar ibn Abdul Aziz ulivyoondoa umasikini huko Afrika Kaskazini hadi kufikia kiwango kwamba hakuna mtu aliyeweza kupatikana kupokea zaka.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: «مَثَلُ الْمُؤْمِنِينَ فِي تَوَادِّهِمْ وَتَرَاحُمِهِمْ وَتَعَاطُفِهِمْ مَثَلُ الْجَسَدِ إِذَا اشْتَكَى مِنْهُ عُضْوٌ تَدَاعَى لَهُ سَائِرُ الْجَسَدِ بِالسَّهَرِ وَالْحُمَّى» “Mfano wa Waumini katika kupendana kwao na kuhurumiana kwao ni kama mfano wa mwili mmoja. Kiungo chochote kinapokuwa na maumivu, mwili wote huitikia kwa kukosa usingizi na homa.” [Sahih Muslim] Ummah wetu nchini Sudan uko katika uchungu. Huenda ulimwengu usijali—lakini sisi ni lazima.

Kitengo cha Wanawake katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir inawataka Waislamu wote kuhamasisha, kukataa masuluhisho ya kirongo, na kulingania kusimamishwa tena kwa haraka Dola ya Khilafah kwa njia ya Utume.

[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اسْتَجِيبُواْ لِلّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُم لِمَا يُحْيِيكُمْ]

“Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele.” [Surah Al-Anfal: 24]

#أزمة_السودان

#SudanCrisis

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Yasmin Malik
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu