- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Mambo Muhimu Kuhusu Ziara ya Rais wa Syria, Ahmad al-Shara, jijini Moscow
Na: Ustadh Ahmad Al-Sourani
(Imetafsiriwa)
Gazeti la Al-Rayah - Toleo 570 - 22/10/2025 M
Rais wa mpito wa Syria, Ahmad al-Sharaa, akifuatana na ujumbe rasmi uliojumuisha waziri wake wa mambo ya nje, Asaad Al-Shaibani, walizuru mji mkuu wa Urusi, Moscow, mnamo 15 Oktoba 2025. Walikutana na Rais wa Urusi Putin katika ziara yao ya kwanza rasmi tangu kuanguka kwa utawala wa Assad, mwishoni mwa mwaka jana.
Yeyote anayefuatilia habari za ziara hii anatambua kwamba haina uhusiano wowote na matakwa ya kuhamishwa kwa Bashar, kama wengine wanavyodai. Inafanyika tu kwa idhini ya Marekani ili kumpa uhalali zaidi Ahmad al-Sharaa, ambaye ana mahusiano tofauti tofauti. Suala la kambi za Urusi nchini Syria, na kuendelea kuwepo kwao, lilijadiliwa, na inaonekana kwamba wameahidi kuendelea kuwepo kwao. Hata hivyo, moja ya athari hatari zaidi za ziara hiyo ni kwamba inaonyesha kwamba kinachofuata baada ya mapinduzi sio kile kilichokuja kabla yake, na kwamba hatua mpya inahitaji kuyasahau mapinduzi na mambo yake ya kudumu.
Ingawa Urusi, ikiongozwa na Putin, ilicheza dori muhimu katika kuimarisha utawala wa Assad kwa miaka kumi kufuatia uingiliaji wake wa kijeshi mnamo 2015 kwa amri ya Obama, ikiuunga mkono kwa silaha, vifaa, na wataalamu na kufanya mauaji mabaya zaidi dhidi ya watu wa Syria, uongozi mpya wa Syria ulipuuza historia hii ya uhalifu ya Warusi. Ujumbe wa Syria uliondoka kwenye mkutano ukibadilishana tabasamu na utani na Putin. Ahmed al-Sharaa hata alisisitiza kwamba anaheshimu makubaliano yote ya awali na Urusi.
Huku wimbi la ukosoaji likienea katika ziara hiyo, kauli zake, na majanga yaliyotokana na hayo yaliyowalipa Warusi kwa kuingilia kati kwao Syria, na kupaka chokaa nyuso zao nyeusi, Waziri wa Mambo ya Nje Asaad Al-Shaibani alijaribu kuokoa hali hiyo kwa mahojiano kwenye kituo rasmi cha habari cha Syria, akitangaza, “Serikali ya sasa ya Syria haikubali makubaliano ya awali ya Urusi yaliyohitimishwa na utawala wa Assad, na kwamba yamesimamishwa. Makubaliano haya yote ya awali yanajadiliwa na kutathminiwa upya.” Kutokana na hili, tunaona kiwango cha mkanganyiko wa utawala wa Syria katika kusimamia masuala ya kisiasa, kinyume na matamanio na matarajio ya watu wa Syria, ambao wana uadui mkubwa dhidi ya Urusi. Al-Shaibani hakuweza kutangaza mikataba hii kuwa batili, lakini badala yake aliielezea kama iliyosimamishwa na iliyo wazi kwa mazungumzo na marekebisho! Hii inagongana na kauli za rais wake, Ahmad al-Sharaa, kuhusu heshima ya mikataba iliyohitimishwa na Urusi.
Ni muhimu kuzingatia kwamba Al-Shaibani alitangaza mnamo Januari mwaka huu kwamba washirika wa utawala wa zamani walikuwa na deni la kigeni la dolari bilioni 30. Baada ya wimbi la maandamano dhidi ya kauli yake, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na serikali ya Damascus kuhusu madeni haya, ikionyesha kukiri madeni, ambayo watu wa Syria walilipa kwa damu wakati wote wa mapinduzi. Kisha, inaonekana kwamba watu hawa waliofiwa wanalazimishwa kulipa madeni haya kutoka mifukoni mwao ili kumtuliza adui wa Urusi!
Msemo, “Hakuna uadui wa kudumu baina ya nchi katika siasa,” ni kauli inayogongana na Sharia ya Kiislamu. Mtume (saw) alitangaza uadui dhidi ya nchi zote ambazo zilikuwa vitani, na akagawanya ulimwengu katika Makao ya Uislamu (Dar ul-Islam) na Makao ya Ukafiri (Dar ul-Kufr). Lengo lake lilikuwa kuziteka ardhi za makafiri na kuziunganisha na Dola ya Kiislamu, kuzibadilisha kuwa makaazi ya Uislamu yanayoongozwa na sheria ya Mwenyezi Mungu (swt), na usalama wao ukilindwa kwa usalama wa Waislamu, yaani, kwa nguvu zao za kijeshi.
Licha ya idadi ndogo ya Waislamu, Mtume (saw) aliwasiliana na wafalme na watawala, akiwaonya, «أَسْلِمْ تَسْلَمْ» “Silimu utasalimika.” Hata alipohitimisha mikataba kama vile Mkataba wa Hudaybiyyah, ilikuwa ni makubaliano ya muda yaliyolenga kuwazima Maquraishi kwa muda. Hii ilisaidia katika ushindi wa Khaybar, na kisha Mtume (saw) akarudi kuiteka Makka. Yeye (saw) hakuwahi kukaa na viongozi wa makafiri, akitabasamu na kuwahakikishia kwamba walikuwa salama kutokana na majeshi ya Waislamu, kama inavyotokea sasa kati ya utawala wa Syria na maafisa wa Kiyahudi, Warusi, au Wamarekani!
Ziara hii haiwezi kuhalalishwa, kufafanuliwa, au kutafsiriwa kwa njia yoyote. Mojawapo ya kanuni za mapinduzi ilikuwa ni kukata ushawishi wa nchi zengine kutoka kwa nchi yetu na kuingilia kwao mambo yetu. Ingekuwa sahihi zaidi kuzingatia nguvu ya jukwaa maarufu ambalo juhudi zake, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu (swt), zilituleta Damascus tukiwa washindi, badala ya kutafuta izza kutoka kwa makafiri.
Kuketi pamoja na Urusi, umbile la Kiyahudi, au adui mkubwa zaidi, Amerika, na kujisalimisha kwa maagizo ya Magharibi ni mwendelezo wa mbinu ya utiifu ambayo Amerika inatafuta kulazimisha kwa utawala mpya, ambao unatafuta kuiweka Syria ndani ya mfumo wa kimataifa, kama ilivyokuwa wakati wa enzi ya utawala wa Assad uliokufa. Watu wa ash-Sham hawakuinuka ili kuzaa mfumo wa kisekula unaotii mfumo wa kimataifa. Badala yake, waliinuka ili kufikia haki na kurudisha nyuma dhulma. Hili litatokea tu ikiwa Uislamu utarudi kutawala kama mfumo wa kisiasa, na dola yake itaweka mfumo mpya wa kimataifa, badala ya kuwa sehemu ya mfumo huu fisadi wa kimataifa ambao ni wa kihalifu dhidi ya watu wake.
Leo, Ummah unalinganiwa kuinua kichwa chake juu, kukata mafungamano ya utegemezi kwa Mashariki na Magharibi, na kuregesha utiifu wake kwa Mwenyezi Mungu (swt) pekee, kwa Mtume Wake (saw) na kwa Waislamu. Heshima ya Ummah wa Kiislamu inaweza kuregeshwa tu kupitia ubwana wa Uislamu, na haki duniani, ambayo inaweza kuanzishwa tu na utawala wa Mwenyezi Mungu (swt). Mwamko wa watu wa ash-Sham na Ummah wa Kiislamu utategemea tu Dini ya Kiislamu na kuwepo kwa mradi mpana unaotokana nayo, kwa kusimamisha dola ya Kiislamu, Khilafah Rashida, kwa Njia ya Utume, ambayo itaunganisha safu zao, kukata mikono ya wakoloni kutoka ardhi zao, na kuregesha hadhi yao miongoni mwa mataifa ya dunia, kama Mwenyezi Mungu (swt) alivyokusudia iwe, Ummah mmoja, unaobeba ujumbe wa haki kwa ulimwengu. Mwenyezi Mungu (swt) amesema,
[وَيَقُولُونَ مَتَى هُوَ قُلْ عَسَى أَنْ يَكُونَ قَرِيباً]
“na watasema: Lini hayo? Sema: A'saa yakawa karibu!” [Surah Al-Israa 51].



