Jumamosi, 21 Rabi' al-awwal 1447 | 2025/09/13
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Tofauti Kubwa Kati ya Azimio la Istanbul na Fatwa Zilizotangulia!

(Imetafsiriwa)

Gazeti la Al-Rayah – Toleo 564 - 10/09/2025 M

Na: Ustadh Abdullah Hamad al-Wadi – Ardhi Iliyobarikiwa - Palestina

Mwishoni mwa kongamano lao waliloliita “Gaza ni Jukumu la Kiislamu na la Kibinadamu” lililofanyika jijini Istanbul kwa siku sita la maulamaa, lililoandaliwa na Erdogan, walitoa tamko la mwisho. Walianza na aya za Qur’an kuhusu maandalizi na Jihad katika Njia ya Mwenyezi Mungu (swt), ili kwamba yeyote anayeisoma afikirie kwamba kitakachofuata kingekuwa ni programu ya kivitendo ya jinsi ya kujishughulisha mara moja na Jihad ambayo sio tu inaiondolea Gaza bali pia inaikomboa Palestina na al-Masjid al-Aqsa. Hata hivyo, uhalisia ulikuwa kinyume. Maamuzi, mapendekezo, na wito uliotolewa ulikuja kana kwamba umeandikwa katika lugha ya mfumo wa kimataifa, unaozingatia sheria za kimataifa, ukirejelea mazungumzo ya tawala tiifu kwa Amerika na Magharibi. Inaweza tu kuelezewa kuwa ni jaribio la kutapatapa la kuficha fedheha ya watawala, hasa miongoni mwao Erdogan, baada ya kufeli kwao na kula njama katika kuisaidia Gaza, na baada ya juhudi zao za kuufungia Ummah kwa kila njia ili usitimize wajibu wake.

Hatuwasingizii uongo Maulamaa hawa tunaposema kwamba hatuwezi kujua lipi ni hatari zaidi: yale yaliyojumuisha ndani ya Azimio la Istanbul, au yale yalioachwa! Ili kufafanua hili, na kwa njia ya kulinganisha, tunawasilisha hapa tofauti rahisi kati ya Azimio la Istanbul na fatwa zilizolitangulia haswa tangu Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Tutazitaja kama “fatwa za awali” zilizotolewa na vyombo na maulamaa wanaotambulika, zenye tarehe na maandishi, zilizochapishwa kwa umma na kuthibitishwa. Huu ni ulinganishi adilifu. Kwa upande mmoja, Azimio la Istanbul lililotiwa saini na maulamaa, na kwa upande mwingine, fatwa zilizotangulia zilizotolewa na maulamaa vilevile lakini zikipelekea kwenye misimamo na vitendo tofauti kabisa.

Ama fatwa zilizotangulia iwe zimetolewa na maulamaa wenyewe, au kwa kuitikia wito na maombi kutoka kwa watu wa Gaza na mujahidina wake, waliouomba Ummah, majeshi yake, na maulamaa wake wajiunge na vita vya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa kama vita vya ukombozi kamili, ziliasisiwa juu ya msingi wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume wake (saw). Zilifafanua faradhi ya Shariah ya kuyakusanya majeshi katika Jihad kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (swt) ili kuikomboa kikamilifu Palestina. Zilitangaza faradhi hii ya Shariah kwa Ummah mzima, huku majeshi yakiwa na faradhi kuu ya Shariah, kwani mikononi mwao kuna silaha na nguvu, na katika safu zao kuna askari waliopewa mafunzo. Fatwa hizi pia zilitangaza ni haram kwa askari kuwatii makamanda wao katika kujiepusha na faradhi ya Shariah. Nyengine hata zilihukumu kwamba uasi dhidi ya watawala ulikuwa ni faradhi, kutokana na ushirikiano wao uliothibitishwa na mapuuza, na kuuzuia kwao Ummah usiisaidie Gaza na kuikomboa Palestina.

Fatwa hizi zilisema kwamba khiyana na uzembe wa watawala huleta ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu hapa duniani na kesho Akhera, na kwamba zinakata mafungamano ya utiifu na kuyakataa. Maulamaa walitoa wito kwa Ummah kuvunja vizuizi kwa nguvu na kushiriki Jihad katika Njia ya Mwenyezi Mungu (swt) ili kuisaidia Gaza, bila ya kusubiri ruhusa kutoka kwa watawala. Walisisiza kwamba maombi yao kwa watawala yalikuwa ni jambo la kuacha uthibitisho mbele ya Mwenyezi Mungu (swt), wakijua watawala hawatafanya lolote baada ya usaliti wao wote.

Zaidi ya hayo, fatwa hizo zilijumuisha maneno ya haki ambayo yalizifanya nyoyo za waumini kutetemeka kwa mfano, kwamba Umma na maulamaa wake hawakuweza kustahamili kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu (swt) Siku ya Kiyama kama maadui kwa watu wa Gaza, mujahidina, na wale waliowekwa kwenye mstari wa vita, na kwamba kifo kitakuwa chepesi zaidi juu yao kuliko msimamo huo.

Kwa ufupi, matendo yaliyojengwa juu ya fatwa zilizopita yanausukuma Ummah kuvunja minyororo yake, kuwaondoa watawala wake, kuregesha udhibiti wa nguvu na majeshi yake, na kuandamana kutekeleza faradhi ya Shariah ya Mola wake Mlezi hadi ukombozi kamili wa Palestina, licha ya tawala na vibaraka wake.

Azimio la Istanbul, hata hivyo, halikuwa na miito yoyote ya hii. Halikutoa wito wa kuyakusanya majeshi, wala kuandamana, wala kuvunja minyororo ya Umma kutoka kwa watawala wake, wala hata kuikomboa Palestina! Badala yake, lilitabanni wito wa Erdogan wa kuunda muungano wa Kiislamu unaosifiwa kama “wa kibinadamu” kwa lengo lililoelezwa la “kukomesh uvamizi na kuwafungulia mashtaka wahalifu.” Azimio hilo, ambalo lilifunguliwa kwa kutaja “kimya cha kimataifa na ushirikiano wa kikanda,” liliendelea kutoa wito wa kushirikisha dola na watendaji hao hao wa kimataifa walioshiriki uhalifu huo, na kuwataka kuwashinikiza kuchukua misimamo. Lilitoa wito wa muungano wa kimataifa wa makundi ya haki za binadamu na mabunge, likaomba taasisi za Kikristo zinazoongozwa na Papa, na hata taasisi za Kiyahudi “kuiokoa Gaza”! Lilitoa wito wa kuamsha maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, badala ya kutumia Shariah ya Mwenyezi Mungu (swt) na hukmu Zake za Shariah kuhusu wale wanaowapiga vita Waislamu na kukalia kimabavu ardhi yao.

Ama kwa Waislamu wenyewe, Azimio la Istanbul liliwekea mipaka wajibu wao wa kuchangia fedha na kutenga nusu ya Zakat ya mwaka ujao kuisaidia Gaza, na kuijenga upya baada ya vita badala ya kutoa tangazo la vita vya ukombozi. Wakati wa lilipozungumzia mzingiro, liliufunga wito wake kwa “njia zilizoko”, ikiwemo kusaidia “maboti ya uhuru" ya kiraia, badala ya kutoa wito wa kutuma meli za kijeshi na majeshi.

Azimio hilo pia lililinganisha Sharia ya Kiislamu na sheria ya kimataifa kama maregeleo, wakati wa kutoa wito wa kukata mafungamano na umbile la Kiyahudi, badala ya kutoa wito wa saratani yote kabisa. Lilisisiza utakatifu wa sanamu ya utaifa kwa kuzipa jukumu “dola zilizolengwa” la kukabiliana na mipango ya “Israel Kubwa” pekee.

Lilimalizika kwa kutoa ushahidi wa uwongo mbele ya watu wote, kutoa asante na shukrani kwa Erdogan, likiisifu serikali yake kama “yenye busara.”

Tathmini hii fupi inaonyesha hatua zinazoweza kujengwa juu ya Azimio la Istanbul, sio zaidi ya kukusanya michango na kuwasihi maadui kuacha vita. Baya zaidi, azimio hilo linawaondolea watawala na serikali uhalifu wao wa usaliti na uzembe, na kuacha utekelezaji wa wito wake kwa watawala hao hao, licha ya uhalisia dhahiri wa ulaji njama na ushirikiano wao.

Ingefaa kwa “Maulamaa wa Istanbul,” chini ya Muungano wa Kimataifa wa Maulamaa wa Kiislamu na Wakfu wa Maulamaa wa Kiislamu nchini Uturuki, ambao walikusanyika kwa mamia kwenye meza ya Erdogan, kuchukua misimamo ya kivitendo ambayo ingeuhamasisha Umma wote na majeshi yake katika hatua za haraka, sio tu kuikomboa Gaza na kukomesha vita, bali kuikomboa Palestina yote. Ingelikuwa sahihi kwa misimamo yao kutoa wito kwa watu na askari waachane na kughuriwa kwao na dunia, wakati vyombo vya habari vinapopeperusha kauli zao, ili wawe tayari kusikia maelekezo ya kivitendo ambayo watauelekezea Umma. Hapo, ulimwengu ungeshikilia pumzi zake na makafiri wangetetemeka kwa kutajwa tu mkusanyiko wao. Walakini, ole wao, walikataa kustahiki hilo.

Hatimaye, maswali mawili ambayo lazima yaulizwe kwa kuzingatia matokeo ya Kongamano la Istanbul ni: Je, kongamano hili lilifanyika kweli kusaidia Gaza? Au lilifanywa ili kuavya kitendo chochote cha maana ambacho kingeweza kujengwa juu ya fatwa zilizopita?

Na baada ya Azimio la Istanbul munatarajia adui yetu mbaya aelewe nini kutoka kwetu? Mauaji zaidi, uharibifu, maiti, na uhamishaji? Je, ataelewa chochote zaidi ya kwamba hili ndilo kubwa ambalo Ummah wenye nguvu zaidi ya bilioni mbili unaweza kufanya, au hata kufikiria kufanya?!

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu