- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Je! Uongozi wa Pakistan Ulipotezaje Hadhi Yake Mbele ya India na Trump?!
(Imetafsiriwa)
Gazeti la Al-Rayah – Toleo 555 – 09/07/2025 H
Na: Bilal Al-Muhajir – Wilayah Pakistan
Uongozi wa kisiasa na kijeshi wa Pakistan ulipoteza ushindi uliopatikana na mwewe wa Jeshi lake la Anga, na simba wa jeshi lake la nchi kavu, juu ya India mnamo Mei, ikitoa funzo ambalo India haitalisahau kamwe, kwa kukubali kusitishwa kwa mapigano kati ya nchi hizo mbili. Hii ni licha ya msisitizo wa India kusitisha Mkataba wa Maji wa Indus, na kuinyima Pakistan karibu 80% ya maji ambayo hutiririka kutoka kwa Mto Indus, ambao unatoka China, unapitia India, na kisha kuingia Pakistan. Hii pia ni licha ya kwamba India bado inaendelea kuikalia kimabavu Kashmir... Kisha, baada ya upatanishi wa Rais wa Marekani, Donald Trump kuweka usitishaji vita kati ya pande hizo mbili, na kuiokoa India kutokana na mtego iliyokuwa imejiwekea, kutokana na hesabu potofu ya mienendo ya madaraka, serikali ya Pakistan ilitangaza, mnamo tarehe 21 Juni 2025, uteuzi wake wa Rais wa Marekani Donald Trump kwa ajili ya Tuzo ya Amani ya 2026, ikidai ni kutokana na “kuhusika kwake pamoja na Islamabad na New Delhi ambako kulipunguza hali iliyokuwa ikizorota kwa kasi” kati ya Pakistan na India mwezi Mei.
Taarifa ya serikali ya Pakistan ilisema, "Wakati wa msukosuko mkubwa wa kieneo, Rais Trump alionyesha mtazamo mzuri wa kimkakati na ustadi wa hali ya juu kupitia mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Islamabad na New Delhi ambayo yalipunguza hali inayozidi kuzorota, na hatimaye kupata usitishaji wa mapigano na kuepusha mzozo mpana kati ya dola mbili za kinyuklia ambao ungeweza kusababisha athari mbaya kwa mamilioni ya watu katika eneo hili zaidi.” Taarifa hiyo iliongeza: "Serikali ya Pakistan pia inakubali na kufurahiya sana ofa za dhati za Rais Trump za kusaidia kutatua mzozo wa muda mrefu wa Jammu na Kashmir kati ya India na Pakistan – suala ambalo liko katikati ya ukosefu wa utulivu wa kikanda."
Katika tofauti kubwa kati ya msimamo wa Pakistan, ambao ulidaiwa kuwa wa mshindi katika vita, na msimamo wa India ambao ulipaswa kuwa wa mshindwa, msimamo wa India ulikuwa wa kujiheshimu na kujitegemea zaidi kuliko ule utiifu wa Pakistan. Msemaji Rasmi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India, Randhir Jaiswal, alikataa madai ya Trump kwamba Marekani ilikuwa imetoa motisha ya kibiashara kwa India na Pakistan, badala ya kusitisha uhasama, huku akidokeza kusitisha mahusiano ya kibiashara ikiwa hawatatii. Jaiswal alithibitisha kwamba usitishaji vita ulikuwa uamuzi huru uliofanywa na uongozi wa kijeshi wa nchi zote mbili, bila uingiliaji wowote wa nje. Pakistan haikukanusha taarifa hizi, jambo ambalo linaashiria kwamba uongozi wake wa kijeshi ulisaliti Ummah na kufuja ushindi kwa upande mmoja bila hata kuwepo kwa mpatanishi au tishio lolote kutoka kwa Trump. Tangazo la uteuzi wa Trump pia lilienda sambamba na ziara ya Mkuu wa Jeshi la Pakistan Munir nchini Marekani, na mkutano wake na Trump, katika Ikulu ya White House, siku moja tu kabla ya Marekani na umbile la Kiyahudi kwa pamoja, kushambulia kwa mabomu vinu vitatu vya nyuklia nchini Iran.
Licha ya upinzani mkubwa wa umma nchini Pakistan dhidi ya uteuzi huu, haswa baada ya Trump kuhusika katika kuunga mkono vita dhidi ya Iran na kuendelea kwake kufadhili na kuhami dola ya Kiyahudi, ambayo imeua zaidi ya watu 100,000 huko Gaza, serikali bado inamtaja kama "mtu wa amani"! Vipi mtu ambaye mikono yake inachuruzika damu ya Waislamu apewe cheo cha “mtu wa amani”?!
Kukasirishwa kwa uteuzi huu hata kumesukuma watu kadhaa ndani ya mirengo tawala kuvunja kimya chao na kukemea uamuzi huo. Seneta wa zamani Mushahid Hussain alichapisha kwenye jukwaa X, "Kwa kuwa Trump hawezi tena kuleta amani, lakini kiongozi ambaye ameanzisha vita haramu kimakusudi, serikali [ya] Pakistan sasa lazima ihakiki, kuondoa na kubatilisha uteuzi wake wa Nobel." Kiongozi wa Jamaat-e-Islami, Hafiz Naeem ur Rehman, aliutaja uamuzi huo kuwa ni "fedheha ya kitaifa," akiongeza kuwa Trump anaunga mkono waziwazi mauaji yanayofanywa na umbile la Kiyahudi dhidi ya Wapalestina. Mbunge Ali Muhammad Khan aliitaka serikali kufikiria upya uamuzi huo akitolea mfano uvamizi wa Marekani dhidi ya Iran. Balozi wa zamani wa Pakistan jijini Washington alielezea uteuzi huo kuwa ovyo kisiasa, akisisitiza kwamba hauakisi maoni ya watu wa Pakistan. Ni wazi kwamba serikali ilifanya uamuzi huu kwa kujipendekeza kwa Trump, sio kwa kuheshimu matakwa ya watu, au wao kuwa sehemu ya Umma na uaminifu kwa sababu zake.
Chini ya serikali inayotawaliwa kwa maslahi ya kibinafsi na maslahi finyo, watu kama Mkuu wa Jeshi Munir wanasukuma mbele maslahi yao wenyewe na miamala ya kifedha, wakiungwa mkono na sauti dhaifu kama ile ya balozi wa zamani Javed Hafeez, ambaye alijaribu kuhalalisha uteuzi huo kwa kudai kwamba Pakistan ilipata faida mbili: kwanza, kudumisha uhusiano wa kirafiki na Trump, ambaye huenda kwa mara nyengine tena akapatanisha na India; na pili, inaaibisha India, ambayo inakataa upatanishi wowote wa mtu wa tatu.
Hata hivyo, je, mtu yeyote mwenye akili timamu anaweza kuamini kwamba Trump ni “mtu wa amani” alipoanzisha vita na mauaji makubwa katika Ulimwengu wa Kiislamu ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita baada ya kushika hatamu? Je, ni jambo la busara kufikiri kwamba yeye ni rafiki wa Islamabad, huku akiwa mshirika wa kimkakati wa India? Je, Trump kamwe anaamini katika urafiki na mtu yeyote, wakati anabadilisha misimamo na kauli zake mara moja? Kuna mtu yeyote anaweza kuamini kuwa Trump angetanguliza Waislamu wa Pakistan badala ya Baniani mshirikina India, mshirika wake anayempendelea katika eneo hilo? Na je, kweli India inaaibishwa na uteuzi wa Pakistan wa Trump, au ni ukweli kwamba Pakistan imejidhalilisha kwa kitendo hiki cha fedheha?
[مَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ * أَفَلَا تَذَكَّرُونَ]
“Mna nini? Mnahukumu vipi nyinyi? Hamkumbuki? [Surat As-Saffat 154-5]