Jumamosi, 29 Safar 1447 | 2025/08/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Masharti ya Ufahamu wa Kisiasa na Uundaji wa Sera (Sehemu ya 3)
Dori ya Ramani katika Ufahamu wa Kisiasa
(Imetafsiriwa)

https://www.al-waie.org/archives/article/19891

Jarida la Al-Waie Toleo 468

Mwaka wa 39, Muharram 1447 H sawia na Julai 2025 M

Luqman Harzallah - Palestina

Imesemwa kuwa mwanasiasa asiyejua ramani ya dunia hajui siasa; ramani ya dunia na maarifa yake ni muhimu kwa ufahamu wa kisiasa.

Maelezo yanayohusiana na ramani hayaishii tu katika kujua eneo la nchi ambayo tukio mahususi linalochunguzwa linahusiana. Badala yake, inapanuka hadi kuelewa eneo la nchi kwenye ramani, asili ya jiografia inayohusiana na nchi, asili ya mipaka yake, mafungamano yake na bahari, mafungamano yake na vipengee muhimu vya kijiografia, na kufahamu hali ya ya watu kulingana na idadi ya watu, msongamano wa watu, asili na sifa za idadi ya watu, na umiliki wake wa nishati na teknolojia.

Ni vyema kutambua kwamba kuna makutano kati ya vipengee vya kisiasa na vya kimkakati vya eneo la nchi. Vipengee vya kisiasa husaidia nchi kutengeneza nafasi muhimu ya kimataifa, na kumsaidia mchambuzi kuelewa masuala ya kisiasa na matukio yanayohusiana na nchi. Kuelewa vipengee vya kimkakati vya eneo la nchi kwenye ramani ni muhimu katika uchanganuzi wa kijeshi, na kwa nafasi ya kijeshi ya nchi kuwa thabiti. Makutano hayo yanatokana na ukweli kwamba nguvu ya kisiasa ya nchi inahusishwa na nguvu zake za kijeshi.

Kufahamu eneo la nchi kunahitaji mambo kadhaa, ikiwemo iwapo ni dola ni ya bara, dola ya bahari, au mchanganyiko wa yote mawili. Dola ya bara ni ile ambayo eneo lake la kijiografia liko nchi kavu, na mipaka yake imezungukwa na ardhi, imezungukwa na nchi zengine, isiyo na njia ya bahari. Dola ya bahari ni ile iliyoko baharini, na kwa hivyo mipaka yake imezungukwa na maji ya bahari. Nchi inayochanganya zote mbili ni ile ambayo ina wingi wa bara, yaani, sehemu kubwa ya ardhi, na pwani zilizo wazi kwa bahari.

Nguvu ya dola ya bara ni ya bara, kumaanisha nguvu yake inahusishwa na nguvu za ardhi, upande wa mazingira ya ardhi, njia za usafirishaji na biashara, na nguvu ya ardhini. Nguvu ya dola ya bahari ni ya bahari, kutokana na uwazi wake kwa njia za baharini, uwezo wa meli zake kusafirisha na kupigana vita, upeo wake mpana wa biashara, na uwezo wake mkubwa wa kuwasiliana na watu wengine. Kwa hivyo, dola ya bara haina nguvu ya upangaji wa pembeni, na uwezo wake wa kutengeneza msimamo wa kimataifa wenye ushawishi unabaki kuwa mdogo kuliko ule wa dola zilizo pembeni zaidi. Kuhusu zile dola ambazo zina sifa zote mbili, kuwa na wingi wa bara na wingi wa bahari, uwezo wao wa kutengeneza nafasi ya juu ya kilimwengu uko juu.

Dola za bara ni pamoja na zile zilizo katikati ya mabara, kama vile Afghanistan, Chad, Niger, Bolivia, na Paraguay. Dola za Bahari ni pamoja na Uingereza, Australia, Japan, Ufilipino, na Indonesia. Nchi zenye sifa zote mbili ni pamoja na Marekani, Uhispania, Uturuki, India, Misri, Libya, Algeria, Yemen, ash-Sham, Iran, Pakistan, Ufaransa, Italia, Ujerumani na China. Wingi wa bara wa Urusi ni mkubwa, lakini imeunganishwa na bahari iliyo ganda, na kufanya matumizi yake ya upande wa bahari kuwa ya gharama kubwa sana. Kwa hiyo, imefanya jitihada kubwa katika historia yake yote kufikia bahari ya uvuguvugu, na inaendelea kufanya hivyo, ili kuchukua mwelekeo wa bahari.

Eneo la nchi kwenye ramani linasalia kuwa kipengee muhimu katika kubainisha uzito wake wa kimataifa, iwe kupitia uwezo wake wa kuunganishwa na nchi nyengine, au eneo lake kwenye njia kuu za mawasiliano za kimataifa. Sio nchi zote za bahari zinafanywa kuwa sawa; zile zilizounganishwa na vipengee muhimu vya kijiografia zina uwezekano mkubwa wa kuchukua uzito wa juu wa kimataifa. Vipengee muhimu vya kijiografia ni pamoja na visiwa, milango ya bahari, miinuko, na maeneo yanayoangazia njia za kimataifa za usafirishaji.

Visiwa vina umuhimu mkubwa katika mambo kadhaa. Ikiwa mipaka ya nchi itapanuka na kujumuisha visiwa katika eneo muhimu, na inadhibiti bahari inayoizunguka, inapata ushawishi wa kimataifa. Kwa hivyo, Japan ilitaka kudhibiti Bahari ya Pasifiki, na shambulizi lake kwenye Bandari ya Pearl labda lilichochewa na hamu yake ya kudhibiti Bahari ya Pasifiki. Ingefanikisha hili, ingeweza kuchukua nafasi ya nchi nambari moja kwa urahisi. Ikiwa visiwa haviko kwenye njia za biashara, eneo lao linaweza kuzingatiwa ikiwa ni muhimu kwa kushawishi nchi nyingine. Zinaweza kudhibitiwa na kutumika kama vituo vya kijeshi, kama vile Visiwa vya Solomon kaskazini-mashariki mwa Australia, na Visiwa vya Socotra vilivyo kusini mwa Yemen mkabala na Pembe ya Afrika. Peninsula, kama Crimea, pia zinajumuishwa katika orodha ya visiwa.

Usafiri wa kimataifa wa baharini huchukua njia kupitia bahari kuu, na ikiwa hali italazimisha kubadilisha njia yake, hili sio gumu hata kidogo. Hata hivyo, wakati njia za meli zinapita kwenye milango ya bahari, ni njia zisizo na budi, kwani njia mara nyingi hufungwa kupitia milango hii. Udhibiti wa Uingereza wa Gibraltar na Bab al-Mandab ulifanya hiki kuwa chombo cha ushawishi wake wa kimataifa wakati ilipokuwa dola kuu huko. Mlango wa bahari wa Taiwan, ambao safari 500,000 za baharini hupitia kila mwaka (Asharq Al-Awsat, 21 Agosti, 2023), uliifanya Amerika kugeuza eneo hilo kuwa eneo la ushawishi na msuguano na China, kwa kujishindia serikali inayotawala nchini Taiwan kuwa upande wake. Mlango wa Bahari wa Bosphorus uliifanya Istanbul kuwa eneo lenye ushawishi wa kimataifa, na hivyo kuwafanya Washirika hao kuipa hadhi maalum katika Mkataba wa Lausanne, ambao uliweka bayana kupokonywa nguvu za kijeshi kwa Mlango huo wa Bahari, pamoja na Dardanelles, Bahari ya Marmara, visiwa vya Uturuki, na baadhi ya visiwa vya Ugiriki.

Isthmus ni ukanda mwembamba wa ardhi unaounganisha maeneo mawili makubwa ya ardhi. Mahali ulipo kwenye njia za kimataifa za usafirishaji huufanya kuwa bandari na mahali pa kuegesha meli katika sehemu zote mbili za mwisho, au inaweza kusababisha nchi inayousimamia kuchimba mkondo unaounganisha ncha mbili za ukanda (isthmus) huo. Mifano ya hii ni Mkondo wa Suez, Mkondo wa Panama, na Mkondo wa Kiel. Kabla ya ufunguzi wa Mkondo wa Panama, ukanda wa Tehuantepec ilikuwa ndio njia fupi zaidi kati ya Ghuba la Mexico na Bahari ya Pasifiki.

Ni wazi kwamba ikiwa nchi za bara haziwezi kufikia bahari, zitalazimika kutegemea mataifa ya kati, ya pembezoni zaidi ambayo yanachukua nafasi kati ya bara na bahari. Hata zile nchi zenye ushawishi mdogo wa kimataifa zinatazama suala hili kwa wasiwasi. Ethiopia, kwa mfano, ilihitimisha makubaliano na Jamhuri iliyojitenga ya Somaliland mnamo 2023 kuipatia njia ya kufikia Bahari Nyekundu.

Asili ya jiografia inayohusiana na dola inajumuisha mambo kadhaa ya kimsingi, ikiwemo eneo lake, asili ya mipaka yake, eneo lake la ndani, aina ya ardhi ndani yake, na muundo wake wa asili. Kuhusu asili ya mipaka ya nchi, hakuna sheria maalum inayosimamia asili ya mipaka, iwe imechaguliwa au iliyowekwa na dola. Ni kawaida kwa dola kujieleza kwa mipaka ya asili, kama vile safu za milima, njia za mito, na fuo za bahari. Mipaka inaweza kuwa imetolewa kwa mujibu wa makubaliano na nchi jirani, au kama matokeo ya upanuzi au mkazo kutokana na vita. Hata hivyo, tangu kutokea kwa mfumo mpya wa kilimwengu, mipaka ya kitaifa imechukua tabia takatifu, na suala la upanuzi limekuwa suala la chukizo la kimataifa, au linalohitaji uhalali unaoakisi matakwa ya watu wengi ya kujiunga au kujitenga. Miongoni mwa jiografia inayohusiana na mipaka ni aina ya vituo vya idadi ya watu vilivyo kwenye mpaka. Mipaka mingine inapakana na nchi mbili na kutenganisha watu wawili, wakati mingine inapakana na nchi mbili na kutenganisha watu wamoja katika sehemu mbili, kila sehemu ikiwa ya serikali tofauti. Hii inatusaidia kuelewa uthabiti na upenyaji wa mipaka kutokana na muunganisho au mtengano wa watu hao wawili katika upande wa mpaka. Jiografia ya mpaka inajumuisha kujua nchi zinazopakana na mpaka na kujua hadhi yao ya kimataifa, ambayo hufungua milango ya ushindani, mzozo, vita, utegemezi, au kuchukua eneo muhimu.

Muundo wa asili unahusiana na maumbile ya mazingira ya nchi na rasilimali zilizomo ndani ya jiografia yake. Rasilimali za maji ya ziada ya nchi ni muhimu kwa usalama wake wa maji, na kupungua kwa hifadhi za maji chini ya ardhi ni kiashirio cha hatari. Utajiri wa mafuta na madini ni jambo muhimu katika nchi, unaoziwezesha kujitosheleza katika nishati na viwanda, na hata kuongeza uwezo wao wa kushawishi wengine kupitia rasilimali hizi. Rasilimali za madini na samaki za baharini ni nyenzo muhimu katika utajiri wao na usalama wa chakula. Umbile la udongo, upande wa ukubwa wa ardhi yenye rutuba, na anga tofauti ya jangwa, huathiri nafasi ya nchi katika suala la nguvu ya kweli ya uchumi wake, au kwa maana nyengine, uwezo wake wa uzalishaji. Hii hata huathiri umbile la watu wake.

Eneo la nchi, kama ilivyo katika upana wa eneo hilo, lina thamani katika nyanja kadhaa - mojawapo ni uhusiano kati ya ukubwa wa eneo na idadi ya watu, nyingine kupitia uhusiano kati ya eneo na utajiri, na nyingine kupitia kina cha kimkakati cha nchi. Kipengee hiki cha mwisho ni muhimu sana, hasa katika tukio la kuathiriwa na uvamizi, kwani eneo kubwa hufanya udhibiti wa wavamizi kuwa wa polepole, na labda kuyumba ikiwa uvamizi wao ni uvamizi wa eneo, na sio uvamizi wa vituo vya mamlaka.

Mandhari ya ndani hutoa njia za kimaumbile za ulinzi wa ndani kwa nchi ikiwa ina ardhi ya milima, au kinyume chake ikiwa ina ardhi tambarare. Utofauti wa ardhi pia huchangia utofauti wa uzalishaji katika nchi. Milima ya Ural nchini Urusi ilikuwa kizuizi cha kimaumbile, ambacho nyuma yake upanuzi mkubwa wa mashariki ulilinda Urusi kutokana na kuporomoka, katika tukio ambalo wavamizi walichukua udhibiti wa sehemu yake ya magharibi, sehemu ambayo mji mkuu wa Urusi, Moscow, iko. Kinyume chake, Tambarare ya Ulaya katika Ulaya Mashariki ulifanya nchi zake kuwa korido ya vita na uwanja wa mizozo ya kitamaduni.

Ni muhimu kwa nchi kuwa kwenye bandari za nchi kavu na njia za usafiri. Eneo la Uturuki linaifanya kuwa kiungo kikubwa cha ardhi kati ya Asia na Ulaya, na hivyo, njia za biashara ya nchi kavu kati ya Asia na Ulaya hupitia humo. Hali hiyo hiyo inatekelezeka kwa nchi zilizo kando ya Barabara ya zamani ya Hariri (Silk Road) na Mpango wa Ukanda na Barabara (Belt and Road Initiative), ikijumuisha China, Kazakhstan, Urusi, Belarus, Poland na Ujerumani. Hii imechochea utekelezaji wa miradi mikubwa kando ya njia hizi, ikiwa ni pamoja na reli, bandari za nchi kavu, na mabomba ya mafuta na gesi.

Idadi ya watu, kwa upande mwingine, ni jambo muhimu sana katika nguvu ya dola. Utafiti juu yake unachukua mbinu kadhaa, mojawapo ikiwa ni ukubwa wa idadi ya watu na kasi ya ukuaji. Mwingine huunganisha idadi ya watu na eneo, hivyo huchunguza msongamano wa watu. Nyingine inahusiana na msongamano wa umri wa watu, na nyingine inahusiana na maumbile ya watu. Nchi ambazo zinatamani kutwaa hadhi ya kimataifa zinasukuma kuelekea kuongeza idadi ya watu wao. Hili linaafikiwa kwa kuhimiza idadi ya watu kuzaana, na kutoa manufaa kwa kila mwanafamilia wa ziada, hivyo kuongeza viwango vya uzazi nchini. Mbinu nyingine ni kufidia nakisi ya idadi ya watu kwa uhamiaji, hivyo kuongeza vivutio vinavyosababisha watu kuhamia nchini, hivyo kuongeza idadi ya watu. Hili huchangamsha uchumi, hutoa ulinzi dhidi ya kutoweka kwa watu, na hutoa uwezekano wa kuendeleza miradi mikubwa ambayo inaweza kuhitaji kupigana vita vya gharama kubwa katika masuala ya wafanyikazi, iwe katika suala la maandalizi au katika suala la kuzaa hasara. Msongamano wa watu, kwa upande mwingine, ni kiashiria cha nguvu ya kibinadamu na kiuchumi ya dola, kwani utaona kwamba miji mikubwa zaidi ulimwenguni ni ile inayotoa fursa nyingi za kiuchumi, rasilimali nyingi, shughuli za kifedha, au vituo vya kisiasa. Msongamano wa watu unaonyesha jamii za wazee au vijana. Jamii za vijana zina uwezo wa juu wa uzalishaji na vita, tofauti na jamii za wazee.

Nishati na teknolojia zimekuwa masuala muhimu katika kuunda nguvu ya mataifa, hasa yale ambayo yana, au yanatafuta kufikia, nafasi maarufu ya kimataifa. Nishati na teknolojia zinahusiana. Ingawa nishati inaweza kuainishwa kama rasilimali ya taifa, inaweza pia kupewa uainishaji tofauti. Inaweza kutazamwa katika suala la upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya nishati ya kisukuku na nishati ya nyuklia ndani ya taifa. Inaweza pia kutazamwa katika suala la uwekezaji wa taifa katika rasilimali zake za nishati zilizopo, kama vile uwepo wa visima vya mafuta, mitambo ya kusafisha, vinu vya nyuklia, na kiwango cha uboreshaji katika vinu vya nyuklia. Rasilimali hizi na nyenzo zinazohusiana huchimbwa na kuendeshwa na taifa, au taifa limetoa makubaliano kwa mataifa mengine kufanya hivyo. Kinyume chake, baadhi ya teknolojia ni za kawaida ndani ya taifa na haziathiri uzito wake kwa kiasi kikubwa, huku nyengine ni sababu kuu katika nguvu zake. Hizi ni pamoja na teknolojia ya bati na chuma, viwanda vizito, teknolojia ya kielektroniki, na tasnia ya microchip. Nyingine ni pamoja na akili bandia, ambayo hutumiwa katika tasnia ya kijeshi na shughuli za kijasusi, na teknolojia ya anga na satelaiti. Kuna mifano mingi ya haya. “Ukiritimba” wa Taiwan juu ya tasnia ya microchip umeipa ushawishi wa kimataifa. Kwa maana nyengine, Amerika imeathiri ulimwengu kwa sababu serikali ya Taiwan iko chini ya Amerika, na kwa sababu mfumo wa uendeshaji wa chips za Taiwan ni wa Amerika. Hakika, Amerika hutoa ruzuku kwa makampuni yanayofanya kazi katika uwanja huu nchini Amerika, ikiwa ni pamoja na Intel, ambayo ina miradi ya chip huko Arizona, Ohio, New Mexico, na Oregon, na kampuni ya Taiwan, TSMC, ambayo ina viwanda viwili vinavyoendelea kujengwa karibu na Phoenix (Al Jazeera Net, Januari 28, 2024). Hii ni kuhakikisha tasnia inabaki chini ya udhibiti wake. Zaidi ya hayo, Amerika ina ubora katika kipengee cha programu ya microchips, na imekuwa mbele ya dunia nzima katika uwanja huu, ambayo imesaidia kuimarisha ushawishi wake wa kimataifa. Kwa upande mwingine, maendeleo ya tasnia ya makombora nchini Urusi yameifanya kuwa kweli katika vita. Kombora la Kinzhal na kombora la hypersonic la Oreshnik yametofautisha nguvu za Urusi. Kuhusu tasnia ya kijasusi, Amerika iliikuza hadi kufikia hatua ya kutengeneza ndege wakati wa enzi ya Usovieti zinazoruka katika miinuko ya juu zaidi ya kutogunduliwa na rada, zikiwa na kamera zenye mwonekano wa juu zinazonasa kwa usahihi maeneo yanayohitajika. Kisha ikaendelea katika utengenezaji wa satelaiti za kijasusi zenye kamera zenye mwonekano wa hali ya juu. Tusisahau teknolojia za kisasa katika uchanganuzi wa picha, utambuzi wa sura, na usalama wa mtandao, hadi kufikia hatua ambayo majeshi yake yanapigana kama wadukuzi wa kielektroniki. Ingawa mambo haya hayajanaswa kwenye ramani za kisasa, ni lazima yazingatiwe katika nchi, kama vile malighafi na rasilimali za mafuta zinavyozingatiwa.

Huu ni mukhtasari mfupi wa mkusanyiko wa masuala ambayo ni muhimu kuzingatia unapotazama ramani, ikizingatiwa kuwa baadhi yana ushawishi mkubwa katika kuangazia nguvu ya dola kuliko nyengine. Hakuna sheria moja inayoamua iwapo dola inamiliki sifa fulani zinazoifanya kuwa na nguvu zaidi kuliko nyengine. Badala yake, inachunguza hali jumla ya siasa za kijiografia ya dola na jumla ya sifa zake.

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu