- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Abu Ubaidah Aamir ibn Abdullah ibn Al-Jarrah (ra), Mwaminifu wa Ummah huu
(Imetafsiriwa)
Jarida la Al-Waie Toleo Na. 467
https://www.al-waie.org/archives/article/19860
Abdul Mahmoud Al-Amri – Yemen
Abu Ubaidah Aamir bin Abdullah bin Al-Jarrah Al-Fihri Al-Qurashi (40 Kabla ya Hijra/584 M hadi 18 Baada ya Hijrah/639 M) alikuwa Swahaba (ra) wa Mtume (saw), kamanda wa Kiislamu, na mmoja wa Maswahaba kumi (ra) waliopewa bishara njema ya Pepo. Alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kusilimu.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akampa jina la “Mwaminifu wa Ummah huu,” akasema,
«إِنَّ لِكُلِّ أُمَّةٍ أَمِينًا وَإِنَّ أَمِينَنَا أَيَّتُهَا الْأُمَّةُ أَبُو عُبَيْدَةَ بْنُ الْجَرَّاحِ»
“Hakika kila Umma una mwaminifu, na Mwaminifu katika Ummah huu ni Abu Ubaidah.” [Bukhari]
Hadhi ya Abu Ubaidah (ra) katika Uislamu:
Abu Ubaidah (ra) anachukuliwa kuwa mmoja wa watu mashuhuri katika historia ya Kiislamu na anapewa heshima ya juu na Waislamu. Alikuwa mmoja wa makamanda wa jeshi la Waislamu huko Ash-Sham, na alicheza dori kubwa katika ushindi wake. Alikuwa na hekima katika uongozi wake na alikuwa na cheo kikubwa miongoni mwa Waislamu katika eneo hilo. Aliipa mgongo dunia (zahid) na mchaMungu, alipenda kutenda mema, na aliwapa watu chochote alichoweza. Alikufa huko Ash-Sham kutokana na tauni, na kifo chake kilikuwa msiba kwa Waislamu. Anasalia kuwa nembo ya hekima, kuipa mgongo dunia (zuhd), na uchamungu katika historia ya Uislamu.
Uislamu wa Abu Ubaidah (ra):
Abu Ubaidah (ra) alisilimu katika hatua za mwanzo za Dawah ya Kiislamu. Alihama kwanza kwenda Habasha na kisha Madina. Alishiriki pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) katika Vita vya Badr, na vita vyengine vyote. Alikuwa miongoni mwa wale waliobaki imara kwenye medani ya vita, pale Waislamu waliposhangazwa na mashambulizi ya washirikina Siku ya Uhud.
Abu Ubaidah Aamir ibn Al-Jarrah (ra) alikuwa miongoni mwa watu waliosilimu mapema. Alisilimu mikononi mwa Swahaba Abu Bakr As-Siddiq (ra), ambaye angechagua kwa uangalifu wale aliowaona kuwa wenye hekima na waliokomaa kuwalingania kwenye Dini ya Uislamu. Miongoni mwa watu hawa alikuwemo Abu Ubaidah (ra), ambaye ndani yake Abu Bakr (ra) aliona usafi wa moyo na uamuzi sahihi. Akishajishwa na hili, Abu Bakr (ra) alimlingania kwenye Uislamu.
Abu Ubaidah (ra) haraka akaitikia Dawah yake, na baada ya muda mfupi, akaenda pamoja na Abu Bakr As-Siddiq (ra) na kundi la wengine akiwemo Abdur Rahman bin Awf, Uthman bin Maz’uun, na wengineo kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), ambaye kisha akazungumza nao kuhusu Uislamu na mafundisho yake. Wote walisilimu pamoja kwa wakati mmoja.
Wakati huo, Mtume (saw) alikuwa bado hajaingia kwenye Nyumba ya Al-Arqam ibn Abi Al-Arqam. Abu Ubaidah (ra) alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano wakati huo, umri wa akili kamili na ukomavu.
Abu Ubaidah ibn Al-Jarrah (ra) alikabiliwa na kukataliwa na madhara yale yale ambayo Waislamu wengine walivumilia katika siku za mwanzo za Dawah kwa Uislamu. Alifanya Hijra pamoja na Maswahaba (ra) hadi Habasha wakati wa kuhama mara ya pili. Alipojua kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amepata Bay’ah kutoka kwa Answari, aliregea Makka. Baada ya hapo, alihujuru pamoja na Mtume (saw) na Maswahaba (ra) kwenda Madina. Alikaa na Kulthum ibn Al-Hadm, na Mtume (saw) akaweka udugu baina yake na Muhammad bin Maslamah (ra).
Kisa cha Jihad na Ushujaa wa Abu Ubaidah:
Abu Ubaidah (ra) alijulikana kwa ushujaa wake na kupenda Jihad. Mtume (saw) alikuwa akimtaja kuwa ni “Mwenye Nguvu, Mwaminifu”. Abu Ubaidah alishiriki katika vita na misafara yote pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), hakukosa hata moja. Aliteuliwa kama kamanda wa vikosi vya kijeshi wakati wa Mtume (saw) kutokana na akili yake ya kijeshi na uongozi wenye mafanikio.
Abu Ubaidah (ra) aliendelea na mapigano na ushujaa wake katika zama za Khulafaa' Rashidun (Makhalifa Waongofu). Alishiriki katika Vita vya Uasi na vita dhidi ya Musaylama Muongo. Alikuwa mmoja wa makamanda wa majeshi ya Kiislamu yaliyotumwa kuifungua As-Sham. Alishiriki katika Vita vya Ajnadayn, Vita vya Al-Samawah, na Marj Al-Saffar.
Wakati wa Khilafah ya Umar ibn Al-Khattab (ra), Umar alimteua Abu Ubaidah (ra) kama kamanda badala ya Khalid ibn Al-Walid (ra) kwa ajili ya kuifungua Damascus. Ushindi ulipewa Waislamu, na Abu Ubaidah akafanya mapatano ya amani na watu wa mji huo, akikubali kuwaachia nusu ya mali zao na makanisa.
Tukio la Kutoa Pete Mbili Zilizoingia Usoni mwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) Siku ya Uhud:
Imesimuliwa kwamba wakati wa Vita vya Uhud, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alianguka, na pete mbili kutoka kwenye kofia yake ya chuma, vazi la chuma linalovaliwa chini ya kilemba, zikazama kwenye mashavu yake matukufu. Abu Ubaidah (ra) alikuwepo, kwani alikuwa ni miongoni mwa Maswahaba waliobaki imara mpaka mwisho wa vita. Akazitoa pete hizo mbili kwenye uso wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwa kutumia meno yake. Kwa kufanya hivyo, meno yake yalimtoka, na akawa mtu aliyevunjika meno ya mbele. Hata hivyo, hii ilizidisha tu uzuri wake na neema, na hakuna aliyekuwa mzuri zaidi ya Abu Ubaidah (ra) mwenye meno yake yaliyovunjika.
Uchamungu na Unyenyekevu wa Abu Ubaidah (ra):
Swahaba Abu Ubaidah (ra) alikuwa mnyenyekevu, na uongozi au majeshi yenye amri hayakumfanya kuwa na jeuri au kiburi. Imepokewa kwamba siku moja alisema, "Enyi watu! Mimi ni Mquraishi, na kama yeyote kati yenu, mwekundu au mweusi, atanipita katika uchamungu, ningetamani kuwa ndani ya ngozi yake."
Mojawapo ya matukio ambayo yanaakisi unyenyekevu wake ni pale Abu Bakr (ra) alipotuma watu wa kumsaidia wakati wa mzingiro wa As-Sham na akamteua Khalid ibn Al-Walid (ra) kuwa kamanda wao. Abu Ubaidah (ra) alimkaribisha kwa uchangamfu na, kutokana na unyenyekevu, alimpa Khalid nafasi yake stahiki na mamlaka.
Uongozi wa Abu Ubaidah juu ya Maswahaba (ra), Hekima Yake, na Utiifu kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw): Imepokewa kwamba katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), Waislamu walianzisha kampeni ya Dhat al-Salasil kwenye viunga vya Ash-Sham. Amiri wa msafara huo alikuwa ni Swahaba Amr ibn Al-As (ra), ambaye alituma kwa Mtume (saw) kuomba aimarishwe.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) aliwachagua baadhi ya maswahaba mashuhuri kwa ajili ya ujumbe huu miongoni mwao Abu Bakr As-Siddiq na Umar ibn Al-Khattab (ra) pamoja na Muhajirun wengine wengi. Alimteua Abu Ubaidah ibn Al-Jarrah (ra) kuwa kamanda juu yao wote.
Hii inaashiria kwamba Mtume (saw) aliona kwa Abu Ubaidah (ra) hekima na uwezo wa kushika wadhifa huo. Abu Ubaidah (ra) hakujibu chochote isipokuwa utiifu kamili na uaminifu kwa Mtume wake (saw).
Wakati wa Khilafah ya Abu Bakr As-Siddiq (ra), Abu Ubaidah (ra) alikuwa mmoja wa makamanda wanne walioteuliwa na Abu Bakr (ra) kuongoza ufunguzi wa Ash-Sham. Baadaye, Abu Bakr (ra) alimuamuru Khalid ibn Al-Walid (ra) kuhama kutoka Iraq hadi Ash-Sham kuchukua amri ya majeshi ya Waislamu huko.
Wakati Umar ibn Al-Khattab (ra) alipokuwa Khalifa, alimuondoa Khalid bin Al-Walid (ra) na akamteua Abu Ubaidah (ra) badala yake. Hapo Khalid (ra) akasema: “Mwaminifu katika Ummah huu ameteuliwa juu yenu.”
Abu Ubaidah (ra) aliongoza kwa mafanikio Ufunguzi wa Damascus na miji mingine na vijiji kote Ash-Sham. Katika mwaka wa 18 H, sawia na 639 M, alikufa kutokana na tauni ya Amwas katika Bonde la Jordan, ambako pia alizikwa.
Mama yake:
Umaymah binti Ghanm bin Jabir, na kwa mujibu wa Jamharat Ansab al-Arab cha Ibn Hazm al-Andalusi: Umaymah binti Uthman bin Jabir bin Abd al-Uzza bin Amirah bin Umayrah bin Wadi‘ah bin al-Harith bin Fihr.
Ibn Hajar ameripoti kwamba mama yake Abu Ubaidah aliishi ili kushuhudia ujio wa Uislamu na akasilimu.
Vyanzo vya kihistoria havitaji chochote kuhusu shughuli za Abu Ubaidah katika zama za kabla ya Uislamu (Jahiliyyah). Hivyo, kurekodiwa kwa maisha yake kunaanza tangu siku aliposilimu. Ibn Hisham na wengineo wamesimulia kwamba "alisilimu kabla ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kuingia kwenye Nyumba ya Al-Arqam ibn Abi Al-Arqam."
Al-Bukhari na Muslim wamepokea kutoka kwa Anas bin Malik kwamba Mtume Muhammad (saw) amesema:
«إِنَّ لِكُلِّ أُمَّةٍ أَمِينًا وَإِنَّ أَمِينَنَا أَيَّتُهَا الْأُمَّةُ أَبُو عُبَيْدَةَ بْنُ الْجَرَّاحِ»
“Kila Umma una mwaminifu, na mwaminifu katika Ummah huu ni Abu Ubaidah bin Al-Jarrah”
Ibn Hajar Al-‘Asqalani amesema, “Mwaminifu (al-Amiin) ni mtu anayetegemewa na mwenye kusifiwa. Ingawa sifa hii ilishirikiwa na wengine pia, muktadha unapendekeza kwamba Abu Ubaidah (ra) alikuwa na daraja la ziada juu ya wengine kama vile unyenyekevu kwa Uthman, hekima ya kimahakama kwa Ali, na kadhalika.”
Tukio la jina hili, kama ilivyosimuliwa na Al-Bukhari, ni kama ifuatavyo: Viongozi wawili wa Najran, Al-‘Aqib na As-Sayyid, walikuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) wakikusudia kushiriki katika mubahala (kuomba laana ya Mwenyezi Mungu kwa pamoja juu ya waongo). Mmoja wao akamwambia mwenziwe: “Msifanye hivyo. Wallahi, ikiwa kweli yeye ni Mtume na tukashiriki naye katika mubahala, sisi na dhuria zetu hatutafaulu.”
Basi wakamwambia Mtume (saw): “Tutakupa utakalotuomba. Tuma tu pamoja nasi mtu mwaminifu, usitume pamoja nasi ila mtu mwaminifu.” Mtume (saw) akajibu, «لَأَبْعَثَنَّ مَعَكُمْ رَجُلًا أَمِينًا حَقَّ أَمِينٍ» “Hakika nitakutumieni pamoja nanyi mtu mwaminifu haki ya uaminifu.” Maswahaba walitarajia kwa shauku kuwa atakuwa mmoja wao. Kisha Mtume (saw) akasema, «قُمْ يَا أَبَا عُبَيْدَةَ» “Simama ewe Abu Ubaidah bin Al-Jarrah.” Na aliposimama, Mtume (saw) akasema:
«هَذَا أَمِينُ هَذِهِ الْأُمَّةِ» “Huyu ndiye Mwaminifu katika Ummah huu.”
Muslim pia amesimulia kutoka kwa Anas kwamba watu wa Yemen walipokuja kwa Mtume (saw) na wakasema, “Tutumie mtu atufundishe Sunnah na Uislamu,” alishika mkono wa Abu Ubaidah na akasema, «هَذَا أَمِينُ هَذِهِ الْأُمَّةِ» “Huyu ndiye mwaminifu katika Ummah huu.”
Kujiepusha Kwake na dunia (zuhd): غَيَّرتنا الدنيا كُلَّنا غَيْرَك يا أبا عبيدة "Dunia ilitubadilisha sisi sote isipokuwa wewe, ewe Abu Ubaidah." (Umar bin Al-Khattab)
Kundi la wasimuliaji liliripoti: Wakati Umar (ra) alipofika Ash-Sham, makamanda na watu mashuhuri walitoka kumpokea. Akasema: Yuko wapi ndugu yangu Abu Ubaidah? Wakajibu: “Yuko njiani.” Kisha Abu Ubaidah (ra) akafika, akiwa amepanda ngamia amefungwa kwa kamba. Alimsalimia Umar (ra), kisha akawaambia watu, “Tuacheni.” Hivyo wakatembea pamoja mpaka walipofika nyumbani kwa Abu Ubaidah. Umar (ra) aliingia na hakukuta kitu ndani ya nyumba isipokuwa upanga wake, ngao yake na tandiko. Umar (ra) akamwambia, “Ungeweza kupata baadhi ya vyombo au kitu (kwa ajili ya starehe).” Abu Ubaidah (ra) akajibu, “Ewe Amir ul-Muminin, hivi vinatosha kutufikisha kwenye hatima yetu ya mwisho.”
Katika riwaya kama hiyo kutoka katika riwaya nyingine: Wakati Umar alipofika Ash-Sham, alimwambia Abu Ubaidah (ra): “Nipeleke nyumbani kwako.” Abu Ubaidah (ra) akajibu: “Ukafanye nini kwangu? Wakaingia, na Umar (ra) hakuona kitu pale. Akasema, "Ziko wapi samani zako? Sioni chochote ila mkeka wa sufi, sahani, na mfuko wa maji iliotengenezwa kwa ngozi. Na wewe ni kamanda! Una chakula chochote?"
Abu Ubaidah (ra) kisha akasimama, akaenda kwenye jawnah (chombo kinachofanana na kikapu au mtungi unaotumika kuhifadhia mikate), na akatoa vipande vichache. Umar (ra) alianza kulia. Abu Ubaidah (ra) akasema: “Je, sikukuambia kwamba utayafanya macho yako yanililie ewe Amir ul-Muminin? Umar (ra) akajibu, غَيَّرتنا الدنيا كُلَّنا غَيْرَك يا أبا عبيدة “Dunia imetubadilisha sisi sote isipokuwa wewe, ewe Abu Ubaidah.”
Al-Dhahabi ameeleza, “Abu Dawud aliandika haya katika Sunan yake na akasema, “Wallahi huku ni kujiepusha na dunia (zuhd) kweli sio kujiepusha kwa mtu masikini na fukara.”
Ibn Sa’d amesimulia kutoka kwa Malik kwamba Umar (ra) alimtuma Abu Ubaidah (ra) ama dinari elfu nne au mia nne na akamwambia mjumbe huyo: “Tazama anachofanya nazo. Kwa hiyo Abu Ubaidah (ra) alizigawanya zote. Kisha Umar (ra) akapeleka kiasi kile kile kwa Mu’adh ibn Jabal (ra), naye pia akagawanya isipokuwa sehemu ndogo, ambayo mke wake alimuomba aziweke, akisema, “Tunazihitajia.” Pindi Mjumbe huyo alipomripotia Umar (ra) haya, alisema: “Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye amewaweka miongoni mwa Waislamu wale wanaofanya mambo kama hayo.”
Upokezi wake wa Hadith
Abu Ubaidah (ra) alisilimu mapema katika ujumbe wa Mtume na alikuwa na elimu kubwa ya Qur'an na Sunnah. Hata hivyo, vitabu vya Hadith vimehifadhi riwaya chache tu kutoka kwake. Sahih al-Bukhari haina hadith zinazonasibishwa moja kwa moja na Abu Ubaidah (ra). Sahih Muslim inanakili hadith moja, na Jami‘ al-Tirmidhi pia anasimulia hadith moja.
Katika Musnad Imam Ahmad, kuna hadith kumi na mbili, lakini baada ya kuondoa marudio, ni hadith saba tu za kipekee zilizobaki. Musnad Abu Ya‘la ina hadith tisa, sita kati yake zinafanana na za mkusanyiko wa Imam Ahmad, na tatu kati yake ni sehemu za riwaya moja iliyopanuliwa.
Hivyo basi, jumla ya riwaya kutoka kwa Abu Ubaidah (ra) inafikia hadith nane, baadhi yake ni mursal (iliyosimuliwa bila ya Swahaba) na nyingine zimeunganishwa (musnad). Baadhi ya silsila zilizounganishwa ni sahih, wakati nyengine ni dhaifu.
Maulamaa wameeleza sababu ya idadi ndogo ya Hadith zilizoripotiwa kutoka kwa Abu Ubaidah (ra) na Maswahaba wengine waandamizi (ra). Ibn Sa‘d amemnukuu Muhammad bin Umar al-Aslami ambaye amesema: “Riwaya kutoka kwa Maswahaba waandamizi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ni chache kwa sababu walifariki kabla ya kuwepo haja kubwa ya riwaya zao. Hadith ni nyingi zaidi kutoka kwa mfano wa Umar ibn al-Khattab (ra) na Ali ibn Abi Talib (ra) kwa sababu walitawala, na waliulizwa maswali na kutoa hukmu.
Maswahaba wote wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) walikuwa viongozi na mifano ya kuigwa, na walichofanya kilihifadhiwa. Waliombwa shauri na wakatoa fatwa, na wakasikia hadith na kuzifikisha.
Hata hivyo, Maswahaba wakubwa (ra) kama vile Abu Bakr, Uthman, Talha, Az-Zubayr, Abu Ubaidah ibn al-Jarrah, na wengineo kama wao, walisimulia kidogo kuliko maswahaba wadogo, kama Jabir ibn Abdullah, Abu Sa‘id al-Khudri, na Abu Hurayrah.
Maswahaba hawa wadogo (ra) waliishi maisha marefu zaidi, walikuwa wakiulizwa mara kwa mara, na watu walikuwa na haja kubwa ya riwaya, ndiyo maana riwaya nyingi na elimu ya Kiislamu ilitoka kwao na wenzao miongoni mwa Maswahaba (ra) wa Mtume (saw).”
Kifo cha Abu Ubaidah (ra):
Abu Ubaidah ibn al-Jarrah (ra) alipatwa na tauni wakati wa Khilafah ya Umar ibn al-Khattab (ra). Wakati Umar (ra) alipojua hili, alihofia usalama wa Abu Ubaidah na akamtumia barua, akiomba aje kwake kwa kisingizio cha kazi muhimu.
Hata hivyo, Abu Ubaidah (ra) alielewa kwamba nia ya kweli ya Umar haikuwa kazi, bali ni hamu ya kumuokoa kutokana na maradhi, kutokana na kuhofia maisha yake akijua ni kwa kiasi gani Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) alimpenda. Ni kwa sababu hii kwamba Abu Ubaidah (ra) alikataa ombi hilo, na badala ya kuomba radhi.
Sababu ya kukataa kwake ilikuwa ni kufuata maagizo ya Mtume (saw) kwamba kama tauni itaenea katika ardhi, wakaazi wake wasiondoke humo. Na kwa hivyo, Abu Ubaidah (ra) alibaki na hatimaye akafa kutokana na tauni ya Amwas, katika eneo la Beisan katika Jordan ya leo. Swala ya janaza iliongozwa na Swahaba Mu‘adh ibn Jabal (ra). Hili lilifanyika katika mwaka wa 18 H (639 M). Wakati wa kifo chake, Abu Ubaidah (ra) alikuwa na umri wa miaka 58.
Watoto Wake:
Ibn Sa‘d amesema, “Abu Ubaidah (ra) alikuwa na watoto wawili: Yazid na Umair.Mama yao alikuwa ni Hind bint Jabir bin Wahb bin Dibab bin Hujayr bin Abd bin Mu‘ayyis bin Amir bin Lu’ayy. Hata hivyo, watoto wa Abu Ubaidah walifariki dunia mapema. (yaani, walikufa wakiwa wadogo), na kizazi chake kikakatika.”
Mus‘ab al-Zubayri pia alisema katika Nasab Quraish, “Kizazi cha Abu Ubaidah ibn al-Jarrah (ra) na ndugu zake kikaondoka.”