- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Uhakiki wa Habari 19/08/2026
Dirisha la Mazungumzo la Siku 60 kati ya Marekani na Iran Laisha
Dirisha la mazungumzo la siku 60 chini ya mkataba wa makubaliano kati ya Marekani na Iran liliisha mnamo tarehe 17 Agosti bila maendeleo yoyote makubwa kuhusu Mlango wa Hormuz. Iran imeweka makataa ya wiki kadhaa kwa Marekani kutekeleza mkataba huo kikamilifu na imetangaza mabadiliko katika sera yake "kutoka ulinzi hadi mashambulizi kamili." Rais Trump alisema Marekani haitajaribu kuongeza muda wa mkataba huo, akisema, "Sina ratiba, sina haraka." Trump pia alitishia kushambulia Oman ikiwa "itazuia" juhudi za Marekani kufungua tena Mlango huo. Wizara ya mambo ya nje ya Iran ilisema haitarekebisha sera yake chini ya "shinikizo, masharti ya mwisho au mipaka ya muda."
Shutma za Waarabu dhidi ya Israel Zaambulia Patupu Huku Vifo vya Gaza Vikiongezeka
Mawaziri wa mambo ya nje kutoka Misri, Qatar, Jordan, Imarati, Indonesia, Pakistan, Uturuki na Saudi Arabia walitoa taarifa ya pamoja mnamo tarehe 16 Agosti wakilaani vikali 'Israel' kukataa mpango wa amani wa Gaza unaoungwa mkono na Marekani, wakitangaza kwamba 'Israel' ina "wajibu wa moja kwa moja na kamili" kwa matokeo hayo. Hata hivyo ndani ya masaa 48, ndege za kivita zilishambulia mgahawa mmoja katika eneo la bandari ya magharibi mwa Jiji la Gaza, na kuwaua Wapalestina sita akiwemo mtoto mmoja na kuwajeruhi wengine 14. Jeshi la umbile la Kiyahudi lilisema liliwalenga makamanda wa Hamas. Mjumbe wa Marekani Kushner alikutana na Netanyahu mnamo Agosti 17, huku Washington ikiripotiwa kuruhusu umbile la Kiyahudi "kwa muda" kuendelea na mashambulizi yaliyolengwa, na huku miji mikuu ya Kiarabu inayohudumia maslahi ya Magharibi ikiendelea kutoa taarifa tupu.
Trump Aamuru Kupunguzwa kwa Mazoezi ya Marekani na Korea Kusini
Mnamo Agosti 16, Rais Trump alichapisha kwamba alikuwa amemwagiza Waziri wa Ulinzi Hegseth "kupunguza kwa kiasi kikubwa" mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini. Mazoezi ya "Ulchi Freedom Shield" yalikuwa yameanza mnamo Agosti 17 kama ilivyopangwa. Kufuatia mkutano wa dharura mnamo Agosti 18, wanajeshi wa Marekani na Korea Kusini walikubaliana kupunguza ratiba ya mazoezi kwa takriban nusu, kufutilia mbali mazoezi ya awamu ya pili ya kukabiliana na mashambulizi na kumaliza mazoezi wiki hii badala ya Agosti 27. Maafisa wa Korea Kusini walisema hawakuarifiwa kuhusu uamuzi wa Trump hapo awali. Kusitishwa kwa shughuli za kijeshi katikati ya mazoezi kumezua wasiwasi jijini Seoul kuhusu mchakato wa mpito wa udhibiti wa uendeshaji wakati wa vita. Trump alitaja gharama kubwa iliyobebwa na Marekani na kubainisha kuwa Korea Kusini "haisaidii" katika kukabiliana na Iran. Uamuzi huo, uliofanywa bila kushauriana na mshirika, unasisitiza udhibiti wa upande mmoja wa Washington juu ya muungano huo.
Marekani Yatuma Orodha ya Maswali ya "Uaminifu" kwa Washirika wa NATO
Marekani imesambaza orodha ya maswali kwa wanachama wa NATO wanaotathmini "uaminifu" wao kwa sera za utawala wa Trump kabla ya kuamua kuhusu kupunguzwa kwa usaidizi wa kijeshi. Hati hiyo inauliza iwapo kila nchi "imekuwa ikiunga mkono hadharani" sera ya kigeni ya Marekani, ni "vikwazo" gani imeweka kwenye ufikiaji wa kambi ya kijeshi ya Marekani, iwapo inanunua kutoka kwa wakandarasi wa ulinzi wa Marekani, na iwapo imepinga sera "zilizotengenezwa Ulaya". Maswali maalum yanarejelea kampeni za kijeshi za Marekani nchini Iran na Ulimwengu wa Magharibi. Washirika wa Marekani wamekataa kile wanachokiona kama jaribio la kulazimisha mpangilio wa kifikra badala ya ulinzi wa Marekani. Orodha hiyo ya maswali inawasili wiki kadhaa baada ya uhakiki wa miezi sita ya uwepo wa kijeshi wa Marekani barani Ulaya, unaotarajiwa kukamilika ifikapo Disemba.
Zaidi ya Wacanada 220,000 Waomba Kufukuzwa kwa Balozi wa Marekani
Zaidi ya Wacanada 223,000 wamesaini ombi la bunge wakidai kufukuzwa kwa Balozi wa Marekani Pete Hoekstra. Ombi hilo linamtuhumu Hoekstra kwa kutoa matamshi yanayoharibu uhusiano wa pande mbili na kuingilia masuala ya ndani ya Canada, ikiwa ni pamoja na "kusawazisha" vitisho vya Trump vya kuiunganisha Canada kama "jimbo la 51." Linaitaka serikali kumtangaza Hoekstra kama mtu asiyetakikana tena nchini humo na kuanzisha uchunguzi kuhusu "uingiliaji kati wa kidiplomasia" wa Marekani. Ombi hilo ni mojawapo ya yaliyosainiwa zaidi katika historia ya mfumo wa maombi kupitia barua pepe wa Canada. Ingawa wachambuzi wanasema serikali haitaweza kumfukuza balozi huyo, ombi hilo linatuma ishara isiyokoseka ya hasira ya watu. Sera za Trump za muhula wa pili, ambazo zinajumuisha ushuru mkubwa kwa bidhaa za Canada na vitisho vya mara kwa mara vya kuiunganisha, zimesababisha kuzorota kwa kasi kwa mahusiano, na safari za Canada kwenda Marekani zimepungua kwa kiasi kikubwa, zikionyesha hisia zinazoongezeka za "kujiepusha na Amerika".
Marekani Yapanua Kampeni ya Kijeshi Amerika Kusini
Utawala wa Trump unapanua kampeni yake ya kijeshi Amerika Kusini kutoka mashambulizi ya baharini hadi operesheni za ardhini katika mataifa washirika ikiwemo Colombia, Guatemala na Honduras. Katika mwaka uliopita, vikosi vya Marekani vimeshambulia boti zinazoshutumiwa kwa biashara ya dawa za kulevya katika pwani za Karibia na Pasifiki, na kuua mamia ya watu. Sasa Washington inatafuta kuwaweka wanajeshi wa Marekani uwanjani kote katika eneo hilo. Waziri wa Ulinzi Hegseth alitangaza upanuzi huo wakati wa ziara yake Panama wiki iliyopita, ambapo alishuhudia mazoezi ya kijeshi ya kimataifa yanayofadhiliwa na Marekani. Operesheni hizo, zinazofanywa chini ya muongozo wa kupambana na dawa za kulevya, zinawakilisha marudio ya kisasa ya Mafunzo ya Monroe ambapo Marekani inaweka chini yake matakwa yake kwa nguvu za kijeshi kote katika eneo hilo.



