- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Kuibuka kwa Miungano Miwili Mipya ya Kijeshi katika Mashariki ya Kati, Caucasus, na Asia ya Kusini
Gazeti la Al-Rayah – Toleo 553 – 25/06/2025 H
(Imetafsiriwa)
Na: Ahmad Al-Khatwani
Muungano kati ya Pakistan, Uturuki na Azerbaijan umekuwa ukichukua umbo kwa utaratibu uliopangwa, tangu viongozi wa nchi hizo tatu walipokutana kwenye mkutano wa kilele katika msimu wa kiangazi wa 2024. Mkutano huo uliwaleta pamoja Rais wa Uturuki Erdogan, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, na Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev. Uliangazia mahusiano ya kisiasa kati ya dola hizo tatu, na kushughulikia masuala ya kikanda na kimataifa kama vile Gaza, Cyprus, Kashmir, na suala la chuki dhidi ya Uislamu.
Iliamuliwa kuinua ushirikiano wa pande tatu, ambazo hapo awali zilifanya mikutano katika ngazi ya maspika wa mabunge na mawaziri wa mambo ya nje, hadi ngazi ya wakuu wa nchi. Mkazo uliwekwa katika kupanua fursa za ushirikiano kati ya dola hizi tatu, ambayo yalielezwa kuwa mataifa rafiki na ya kindugu. Lengo ni kuimarisha ushirikiano wao kwa njia ambayo inachangia ustawi wa watu wao, na kukuza amani na utulivu wa kikanda na kimataifa.
Mkutano huo ulisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya dola hizo tatu katika kupambana na vitisho vya kimataifa, hasa kile ambacho kimetajwa kuwa ugaidi, na kuthibitisha azma yao ya pamoja ya kukabiliana nalo kama hatari kwa wote.
Kihistoria, uratibu wa Uturuki na Pakistan kuhusu misimamo ya kikanda uliibuka mapema miaka ya 1950, wakati Uturuki ilipoiunga mkono Pakistan kuhusu suala la Kashmir. Baadaye, nchi zote mbili, pamoja na Iraq, zilijiunga na Mkataba wa Baghdad, ambao uliungwa mkono na Uingereza kukabiliana na kibaraka wa Amerika katika eneo hilo, mtawala wa Misri Jamal Abdel Nasser, kama sehemu ya uhasimu wa Marekani na Uingereza juu ya Mashariki ya Kati wakati wa miaka ya 1950.
Hata hivyo, mahusiano halisi ya kijeshi kati ya Pakistan na Uturuki yalianza baada ya 2015, yakihusisha uratibu wa ulinzi kati ya nchi hizo mbili. Uzalishaji wa pamoja wa kijeshi uliongezeka kwa kiasi kikubwa, pamoja na ushirikiano wa kiuchumi hasa katika kuwezesha Njia ya Hariri ya China, kwa ajili ya kusafirisha bidhaa kutoka China hadi Pakistan, kisha Uturuki, na kuendelea hadi Ulaya.
Ama kwa dola za Magharibi, hususan Marekani, ushirikiano huu mkubwa wa pande mbili kati ya dola mbili kubwa na muhimu za kieneo hauleti wasiwasi mkubwa, kwani Uturuki ni mwanachama wa NATO na imejitolea kikamilifu kwa kanuni na masharti ya muungano huo. Hii, kwa upande wake, inaivuta Pakistan katika aina ya utegemezi usio wa moja kwa moja kwa NATO, kwa ufanisi kuiweka chini ya ushawishi zaidi wa Magharibi.
Hata hivyo, kuna hali ya wasiwasi nchini Marekani kuhusu uwiano wa Pakistan na China, kwa gharama ya India, mshirika wa Washington na mwanachama mkuu wa mkutano wa Quad, kambi ya kimataifa ya kisiasa inayojumuisha Marekani, India, Japan na Australia. Hata hivyo, hali hii ya wasiwasi haiathiri kwa kiasi kikubwa kiini cha mahusiano ya kimataifa na Pakistan na Uturuki.
Ili kukabiliana na ukosefu huu wa usawa, hasa baada ya mzozo wa hivi majuzi kati ya India na Pakistan, na kukabiliana na muungano wa Pakistan-Uturuki-Azerbaijan, pamoja na kambi sawia na India, Iran, na Armenia, India ilijibu Uturuki kuipatia Azerbaijan silaha kwa kusambaza silaha kwa Armenia. Hii ilikuja baada ya Urusi kujiondoa katika eneo hilo, kufuatia vita vya Nagorno-Karabakh, na kushindwa kwa Armenia na mpinzani wake Azerbaijan, pamoja na Urusi kuitelekeza Armenia na msimamo wake wa kutoegemea upande wowote.
India kwa hakika imeanza kuongeza mauzo ya nje ya silaha zake kwa Armenia, katika hatua ya wazi inayolenga kukabiliana na kuongezeka kwa muungano wa kimkakati kati ya Uturuki, Azerbaijan na Pakistan. India inauona muungano huu wa pande tatu kama uadui wa wazi dhidi yake, wenye mwelekeo wa kijeshi na kisiasa ulio wazi, ambao unapinga moja kwa moja maslahi yake ya kikanda. India inauona upatanishi huu kama msimamo wazi dhidi yake, haswa baada ya mzozo wa hivi majuzi kati ya India na Pakistan.
Mnamo 2022, mkataba wenye thamani ya dolari milioni 244.7 ulitiwa saini kati ya India na Armenia, ambapo India itaisambazia Armenia Zana ya Kurusha Roketi Nyingi aina ya (MBRL), pamoja na anuwai ya risasi na vifaa vya usaidizi. Mpango huo unakadiriwa kujumuisha betri zisizopungua nne, na pia unashughulikia makombora ya chokaa, makombora ya kukinga vifaru na aina nyinginezo za silaha.
Mnamo 2023, kampuni ya India ya Kalyani Strategic Systems Limited (KSSL) ilitia saini makubaliano ya dolari milioni 155.5 ili kuipatia Armenia bunduki za mizinga 155mm, kama sehemu ya kuimarisha mafungamano ya kijeshi kati ya nchi hizo mbili. Katika mwaka huo huo, haswa mwishoni mwa Oktoba 2023, kampuni ya India ya Zen Technologies, iliyobobea katika mifumo ya uigaji wa kijeshi na teknolojia ya kupambana na droni, ilitangaza uuzaji nje wa vifaa kama hivyo kwenda Armenia vyenye thamani ya dolari milioni 41.5. Mnamo 2024, Armenia ilitia saini mkataba mwingine wa kununua mifumo ya ulinzi ya anga ya Akash kwa idadi isiyojulikana, na kuifanya Armenia kuwa moja ya waagizaji wakubwa wa bidhaa za ulinzi za India, na kuiweka India kama moja ya wasambazaji wakuu wa silaha wa Armenia.
Marekani, bila shaka, inaegemea India zaidi ya Pakistan. Inaweka vikwazo kwa matumizi ya ndege zinazosafirishwa kutoka Marekani kwenda Pakistan, kama vile aina ya F-16 na nyinginezo, kuzuia matumizi yao halisi dhidi ya India. Ndege hizi ni kwa madhumuni ya kujihami tu, au zinaruhusiwa kutumika tu dhidi ya harakati za kijihadi.
Kwa upande wake, Iran inasimama na Armenia na India katika kambi inayopinga mhimili wa Pakistan-Uturuki-Azerbaijan. Hivi majuzi Iran ilizuia mradi wa Ukanda wa Zangezur, uliolenga kuunganisha Uturuki na Azerbaijan na dola za Asia ya Kati, kama vile Kazakhstan, Uzbekistan, Kyrgyzstan, na Turkmenistan. Kwa kufanya hivyo, Iran imezuia njia kwa Uturuki kufikia nchi zinazozungumza Kituruki, zikitumika kama kizuizi cha kijiografia, kuzuia dola hizi kuunda aina yoyote ya umoja au muungano.
Kwa hivyo, miungano miwili inayopingana na yenye uadui ya pande tatu imeundwa katika Mashariki ya Kati, Caucasus, na Asia ya Kusini: muungano wa Pakistan-Uturuki-Azerbaijan dhidi ya muungano wa India-Iran-Armenia. Kila kambi inajumuisha wahusika wakuu wawili wa kikanda, mmoja wao ni serikali ya nyuklia, na nchi moja ndogo, inayohusishwa. Kuundwa kwa kambi hizi kumeunda aina ya usawa wa kikanda, ambayo husaidia kuzuia kukosekana kwa utulivu katika eneo hilo, kufuatia kujiondoa kwa Urusi kutoka kwenye mandhari.