- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Kuwahamasisha Watu Wenye Azma ya Kutimiza Faradhi Yao ya Shariah
(Imetafsiriwa)
Mwenyezi Mungu (swt) asema katika Quran Tukufu, [وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَاناً لِكُلِّ شَيْء ] “Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinacho bainisha kila kitu” [Surah An-Nahl: 89]. Ufafanuzi huu wa kiwahyi unathibitisha kwamba Uislamu si hotuba ya kiroho tu, bali ni mfumo kamili wa maisha. Unaleta imani thabiti inayokinaisha akili na kujaza moyo amani, pamoja na Sheria za Sharia zinazopanga kila kipengee cha maisha ya mwanadamu; iwe katika utawala, uchumi, jamii, siasa, elimu, au mahusiano ya kimataifa. Ni Dini ya haki kwa sababu inatoka kwa Mwenyezi Mungu (swt), na imejengwa juu ya msingi imara; Aqeeda (itikadi) ya Kiislamu, ambayo kwayo mfumo huo unachipuza. Kwa hivyo, uhusiano wa mtu na Uislamu ni wa kiakili na unajengwa juu ya ukinaifu, sio kuiga au hisia. Inaafikiana na umbile kamili la mwanadamu na inavutia akili. Wale wanaouamini kwa utambuzi hawawezi kujizuia kubeba Dawah kwa wengine, wakijitahidi kuionyesha na kuitekeleza. Kubeba Dawah ya Uislamu ni faradhi kubwa ya Shariah na jukumu kubwa.
Mwenyezi Mungu (swt) asema, [وَأَنَّ هَذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيماً فَاتَّبِعُوه] “Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyo Nyooka. Basi ifuateni,” [Surah Al-Anaam: 153]. Kwa hivyo, je, tumefuata kile ambacho Mwenyezi Mungu (swt) ametuamuru, hasa kwa vile tumejitolea kubeba amana hii kubwa na kubadilisha uhalisia huu wa dhulma kwa kusimamisha Khilafah Rashida?
Enyi ndugu na dada: tuna jukumu kubwa. Ni amana ya kueneza ujumbe wa Risaalah, kubeba Uislamu, na kusimamisha Uislamu kama mfumo kamili wa maisha kivitendo. Hili ni jukumu la Mitume (as) na urithi wa Mtume wetu mpendwa Muhammad (saw). Mwenyezi Mungu (swt) atatuuliza kuhusu kile tulichokabidhiwa, kwa hivyo tufanye kazi kwa ajili ya siku ambayo utajiri wala watoto hawatakuwa na faida yoyote, isipokuwa wale wanaomjia Mwenyezi Mungu (swt) kwa moyo safi. Ndiyo, leo ni wakati wa kutenda, sio kuhukumiwa, na kesho itakuwa siku ya hukumu, bila vitendo zaidi kuwezekana. Leo, tunaulizwa: Je, tumefikisha ujumbe wa Mola wetu? Je, tulifuata njia ya mabadiliko kama Mwenyezi Mungu (swt) alivyoamuru? Je, tulibaki imara katika mfumo, bila kulegeza msimamo au kurudi nyuma? Kila kitu ni cha muda mfupi, mamlaka ni ya muda, na nguvu hatimaye zitafifia. Mwenyezi Mungu (swt) amesema, [وَيَبْقَى وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ] “Na atabakia Mwenyewe Mola wako Mlezi Mwenye utukufu na ukarimu.” [Surah Ar-Rahman: 27].
Enyi watukufu: Mnafikiria nini kuhusu tukio la Siku ya Kukusanyika (Siku ya Kiyama)? Siku hiyo ya kufazaisha na ya kutisha; wakati kila mama anayenyonyesha atakapomsahau mtoto wake, kila mwanamke mjamzito atashusha ujauzito wake, roho zitashtuka, na macho yatalia. Ni siku ya dhiki, udhalilifu, na hofu kubwa. Hakuna atakayeokolewa kutokana nayo isipokuwa wale ambao matendo yao ni ya kweli na kwa mujibu kamili wa amri za Mwenyezi Mungu. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema, «الْكَيِّسُ مَنْ دَانَ نَفْسَهُ وَعَمِلَ لِمَا بَعْدَ الْمَوْتِ، وَالْعَاجِزُ مَنْ أَتْبَعَ نَفْسَهُ هَوَاهَا وَتَمَنَّى عَلَى اللَّهِ» “Mwenye hekima ni yule anayejihisabu nafsi yake na akafanya kazi kwa yale yanayokuja baada ya kufa, na mpumbavu ni yule anayefuata matamanio nafsi yake na kutarajia kwa Mwenyezi Mungu kheri.”
Basi, enyi wabebaji wa Dawah: nyinyi ambao Mwenyezi Mungu (swt) amewateuwa kuwa askari wake hapa duniani, fanyeni vitendo vyema na sahihi kama alivyoamrisha Mwenyezi Mungu (swt) sio kwa matakwa au maslahi ya dunia. Bakini imara katika njia, takaseni nia zenu, shikamaneni imara na fikra na njia, na muwe na subira kama Mitume (as) wenye azma thabiti walivyokuwa na subira.
Enyi ndugu na dada, hebu na tuwe miongoni mwa wale wanaoacha alama nyuma ambayo haiwezi kufutwa kamwe, wale ambao, kwa maneno yao na damu yao, hutengeneza njia ya Khilafah na ushindi. Kwani njia hii, ingawa inaweza kuwa ndefu, ni njia ya heshima na milele. Kwa hivyo tuimarishe azma yetu na tujiandae kwa akhera (Siku ya Kiyama) mbele ya Mwenyezi Mungu (swt). Dawah kwa Uislamu inatuita, ushindi unakaribia, na Ummah unatusubiri sana.
Enyi ndugu na dada, Enyi wabebaji wa Dawah: sikilizeni hekima iliyosimuliwa kutoka kwa Abu Dharr (Mwenyezi Mungu awe radhi naye): “Ifanyeni upya njia yenu kwenye meli, kwani bahari ni ndefu; chukueni riziki nyingi, kwani safari ni ndefu; takaseni matendo yenu, kwani Hakimu, Mwenyezi Mungu (swt), ni Mwenye kuona yote. Punguzeni mzigo wenu wa Dunia, kwani mawimbi ya milimani ni makali.” Ndiyo, bahari ina kina kirefu, mitihani ni mikali, na watu wamepotea katika mkanganyiko. Hata hivyo, mko kwenye mwongozo kutoka kwa Mola wenu, kwa hivyo iimarisheni meli yenu na ifungeni kwa kamba za imani. Bebeni ndani yake matendo ya dhati tu, kwani mizani ni ya haki, na Hakimu anaona yote.
Tuwe watu wenye matarajio makubwa, wale ambao hawaridhiki kamwe kwa mambo madogo, ambao hawalegezi msimamo juu ya haki (haq), na ambao hawatafuti faraja kwa gharama ya faradhi ya Shariah. Mtu mwenye azma ya kweli ni yule anayejitolea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (swt) ili kusimamisha Dini Yake. Anaiona Khilafah kama ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt), ya uhakika na ya kweli. Anajua kwamba ushindi huja kwa uvumilivu, na kwamba mafanikio ya mwisho ni ya watu wema.
Mwenyezi Mungu (swt) anasema, [إِن تَنصُرُوا اللَّهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ] “Enyi mlio amini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu.” [Surah Muhammad: 7]. Yeyote ambaye Mwenyezi Mungu (swt) anamnusuru hawezi kushindwa, na yeyote ambaye Mwenyezi Mungu atamwacha, atawezaje kufanikiwa? Mbele yetu kuna Ummah unaotamani mabadiliko. Mbele yetu kuna damu na kafara mjini Gaza, vilio kutoka Al-Masjid Al-Aqsa vikiomba msaada, na usaliti unaozunguka ardhi zetu kutoka kila upande. Kwa hivyo, je, tumesimama kwa ajili ya Haki? Je, tumepaza sauti zetu dhidi ya batili? Je, tumehamia kuinusuru Dini ya Mwenyezi Mungu (swt)? Tukumbuke msemo wa Al-Hasan Al-Basri, الدنيا ثلاثة أيام: أما الأمس فقد ذهب بما فيه، وأما الغد فلعلك لا تدركه، وأما اليوم فلك فاعمل فيه “Dunia hii ni siku tatu: Jana imepita na yote yaliyomo. Kesho, huenda usiifikie kamwe. Leo ndiyo yote uliyo nayo, kwa hivyo fanya matendo mema ndani yake.” Ndiyo, leo ni siku yetu, kwa hivyo tufanye matendo mema! Tutumie yaliyobaki katika maisha yetu. Tufanye kazi, kwani tuko kwenye njia ya Mtume wetu (saw), na kwa hakika, Mwenyezi Mungu haachi kamwe thawabu za watendaji mema zipotee.
Enyi ndugu na dada, Enyi wabebaji wa Dawah: Ndiyo, Dawah yetu ni safi na iliyo wazi kama mwanga wa alfajiri, isiyo na mkanganyiko na uchafu. Ujumbe wetu haukujengwa juu ya ukabila na utaifa, wala uhusiano wa nasaba, maslahi ya kimwili, jiografia, au faida ya kidunia. Fungamano letu ni Iman, Dini yetu ni Uislamu, na lengo letu ni radhi za Mwenyezi Mungu (swt), Yule asiye na mshirika. Mtume (saw) amesema, «كُونُوا عِبَادَ اللهِ إِخْوَاناً» “Kuweni waja wa Mwenyezi Mungu, ndugu.” Huu ndio ushauri wake (saw) kwetu, na tunatumaini kuwa miongoni mwa wale wanaoishi kwa huo kweli. Hakika, Uislamu uliwafanya ndugu Ansar na Muhajirun, na wakawa mfano mzuri wa kujitolea na kutokuwa na ubinafsi.
Enyi ndugu na dada: kubeba Dawah sio tu kazi au harakati ya kifikra pekee. Ni kazi ya Manabii (as) na Mitume (as). Inamaanisha kutembea katika nyayo zao, kurithi njia yao. Ni heshima kubwa na jukumu zito. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema, «لَأَنْ يَهْدِيَ اللَّهُ بِكَ رَجُلاً خَيْرٌ لَكَ مِنْ أَنْ يَكُونَ لَكَ حُمْرُ النَّعَمِ» “Kama Mwenyezi Mungu atamwongoza mtu mmoja kupitia wewe, ni bora kwako kuliko kuwa na ngamia wekundu.” Ni watu wangapi leo wanahitaji uongofu? Ni roho ngapi zilizokandamizwa zinasubiri afueni kupitia mikono yetu?! Je, tutaridhika kuishi bila kusudi?! Kuwa idadi nyengine tu maishani?! Maisha yetu yapite na tuulizwe: Mlifanya nini kwa ajili ya Dini yenu na Umma wenu?!
Wallahi, hapana! Tuweni miongoni mwa wa kwanza kuchukua hatua, miongoni mwa wale wanaochukua hatua, watu wanaoanzisha matendo mema yenye athari na ushawishi, si malalamiko na manung’uniko yasiyokwisha; wale wanaojenga, na wale ambao hawaakhirishi, hawanasiti na kusubiri.
Mwenyezi Mungu (swt) alisema, [قُلْ هَٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّهِ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ ] “Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua.” [Surah Yusuf: 108]. Ni njia iliyo wazi, yenye maono na yakini; Dawah ya kusimamisha Dini na kutimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu ya Khilafah kwa Njia ya Utume.
Enyi ndugu na dada: sisi si watu wanaoishi tu kula na kunywa. Sisi ni Umma wa ujumbe, Umma wa uongozi, Umma wa uongofu. Tuchagueni kuwa kama ‘Umar (ra), Saad (ra), Khalid (ra) na Ṣalaḥuddin (rh) … watu waliobadilisha mkondo wa historia, wakiacha nyuma muanga, harufu nzuri, na alama za milele.
Kwa hivyo, ewe msikilizaji wa maneno haya — fanya haraka kuelekea msamaha wa Mola wako. Usiwasikilize wale wanaokukatisha tamaa. Usikengeushwe na sauti za shaka. Kuwa cheche ya matumaini, muanga wa uongofu, na jiwe la ujenzi katika jengo kuu la Uislamu. Mtume (saw) amesema, «إِذَا مَاتَ ابْنُ آدَمَ انْقَطَعَ عَمَلُهُ إِلَّا مِنْ ثَلَاثٍ: صَدَقَةٍ جَارِيَةٍ، أَوْ عِلْمٍ يُنْتَفَعُ بِهِ، أَوْ وَلَدٍ صَالِحٍ يَدْعُو لَهُ» “Anapokufa mwanadamu amali zake hukatika isipokuwa tatu tu: Sadaka yenye kuendelea, elimu yenye manufaa, au mtoto mwema anayemfanyia Dua” (Imepokewa na Muslim). Hadith hii inatukumbusha kwamba kinachobakia kwa hakika kwa mtu baada ya kufa ni wema alioufanya wakati wa uhai wake, matendo yao yenye manufaa ya athari ya kudumu. Dunia hii ni shamba tunalopanda kwa ajili ya Akhera. Tunachopanda leo, tutavuna kesho. Kwa hivyo tujitahidi kuacha maarifa yenye manufaa kwa Ummah, Dawah iliyobarikiwa inayofaidi vizazi vijavyo, na watoto wema wanaoendelea na njia ya haki. Huu ndio uwekezaji halisi, ambao haujawahi kufeli.
Ewe Mwenyezi Mungu, tufanye tuwe miongoni mwa wale wenye kusikia maneno kisha wakafuata yale yaliyo mema.
Ewe Mwenyezi Mungu, tufanye miongoni mwa wale wanaoitikia wito wako, wanaofanya kazi kusimamisha Dini yako, na tubaki imara hadi tushuhudie ushindi kwa macho yetu, au tukutane na Wewe hali ya kuwa uko radhi nasi. Amin.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Abdul Mahmoud Al-Amiri – Wilayah Yemen