Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

Ndiyo, Uko Gaza na Gaza Inaangamizwa!

(Imetafsiriwa)

Habari:

Rais Recep Tayyip Erdoğan alitoa kauli katika mpango wa ufunguzi wa Wiki ya Maulid al-Nabi. Akitoa sehemu kubwa ya hotuba yake kwa Gaza, Erdoğan alielekeza shutuma kali kwa Waziri Mkuu wa “Israel” Netanyahu.

Erdoğan alisema, “Popote palipo na Muislamu duniani, nyoyo na akili zetu ziko pale,” na kuongeza, “Ndio maana sasa tuko Gaza. Hatuwezi kubaki watazamaji wa uasi wa dhalimu huyu, kafiri huyu anayeitwa Netanyahu, huko Palestina hivi sasa.” (NTV, 03/09/2025)

Maoni:

Huku uvamizi na mauaji ya halaiki mjini Gaza, yakiendelea kwa muda wa miezi 23, yamefikia kilele kwa matumizi ya silaha ya njaa inayoangamiza watu pamoja na majaribio ya mbinu mpya za mauaji zinazoitwa “mabomu ya roboti”; siasa za kinyonyaji na za kinafiki za watawala wa nchi za Kiislamu—wanaokabiliwa na ghadhabu za watu wao wenyewe kwa kuitelekeza Gaza—pia zimefikia kilele cha vilele.

Watawala hawa, ambao wamepoteza sio tu kitambulisho chao cha Kiislamu bali hata hisia zao za ubinadamu, wanaendelea na mahusiano yao ya wazi na ya siri na “Israel” bila kukatizwa, huku kwa upande mwengine wakienda mbali zaidi na kudai wanaisaidia Gaza. Ukaidi huo umefikia kiwango ambacho tawala kama vile Misri, ambayo inadumisha kufunga kivuko cha Rafah na kuilaani Gaza kwa njaa na kifo, na Jordan, ambayo inashika nafasi ya kwanza katika kulipatia jeshi la Kiyahudi matunda na mboga mboga, inajinaki kuisaidia Gaza.

Na huyu hapa Rais Erdoğan, akimaanisha chini ya shangwe za wale wanaojiita wazuoni na walimu mbele yake, kwamba Uturuki inaisaidia Gaza kwa siri kwa kusema, “Tuko Gaza hivi sasa.” Hawamuogopi Mwenyezi Mungu wala hawaoni haya mbele ya Umma.

Mwandishi wa habari wa Kipalestina Muhammad Abu Taqiya, ambaye hakuweza kustahamili hata ukatili mkubwa kama huo kugeuzwa kuwa unyonyaji wa kisiasa, alimwambia Erdoğan, “Inatosha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu!” na kuandika mistari ifuatayo:

“Ndiyo, uko Gaza! Ndio maana, kama tunavyoona kwenye video, mujahidina mjini Gaza wanapigana kwa silaha za hali ya juu na zenye ufanisi zaidi!

Ndiyo, uko Gaza… Ndiyo maana watu huru wa dunia wanalazimika kufika Gaza kutoka makumi ya maelfu ya kilomita kutoka Magharibi, kwa njia ya bahari; ilhali Gaza iko umbali wa masaa 11 tu kutoka kwa bahari yako!

Hakuna mji huko Gaza ambao umeharibiwa kabisa na mbele ya macho yako! Kwa sababu uko kule. Huko Gaza, watoto 19,000 hawajauawa kikatili mbashara! Kwa sababu uko Gaza, hakuna mtu aliye weza kufanya hivi! Huko Gaza, wanawake 10,000 hawajaangamizwa bila huruma! Kamwe, maadamu wewe uko kule, hakuna mtu anayeweza kufanya kitu kama hicho!

Uhaba wa vifaa vya matibabu na dawa mjini Gaza sio 80%! Wewe unaleta kila kitu! Mjini  Gaza, watoto 48,000 hawajaachwa yatima! Mbele ya macho ya ulimwengu! Hospitali za Gaza zinafanya shughuli muhimu zaidi na kutoa huduma za afya kwa njia bora zaidi! Kwa uwepo wako, bila shaka, yote haya yanatokea!

Mamia ya watoto na watu wazima mjini Gaza hawajakufa kwa njaa! Hawawezi kufa! Mamia ya watu hawajapoteza maisha kwa ajili ya kipande cha mkate! Kwa sababu wewe mwana Gaza!

Na je hukusema kwamba ‘Msikiti wa Al-Aqsa ni mstari mwekundu kwetu’? Ndio maana katika siku za hivi karibuni, vikosi vya uvamizi, makundi ya Kizayuni, na mawaziri hawajaweza kuivamia Al-Aqsa kwa wingi!

Sasa tafadhali, achana na kauli kama hizo ambazo haziwiani na hata dhamiri yako, achilia mbali Gaza! Achana nazo ili heshima na upendo uliosalia kwako pia zisipotee! Kusema, ‘Nisingeweza kufanya hivyo, nilizungumza makubwa sana wakati huo. Njoo, unishike mkono, tuifute aibu hii pamoja,’ haitakuletea madhara yoyote. Inatosha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu!”

Kwa mistari hii, wacha tuongeze yafuatayo:

Ndiyo, uko Gaza... Ukiwa na mafuta yako, chuma chako, pamoja na meli zako za biashara, zilizo bidhaa zisizohesabika zinazojulikana na zisizojulikana, uko Gaza.

Uko Gaza na saini yako kwenye Azimio la New York, ambalo lilifafanua Oktoba 7 kama “shambulio la kigaidi,” likitaka mujahidina kuweka silaha chini na kujisalimisha, na kufikiria kuacha utawala wa Gaza kwa timu ya msaliti Mahmoud Abbas ili kubadilishana na kijidola cha kindoto cha Palestina kisicho na jeshi au ubwana.

Uko Gaza na dori yako ya upatanishi nchini Azerbajan kwa lengo la kuhalalisha mahusiano ya “Israel” na serikali ya Syria, na hivyo kuzuia jihad ya Waislamu wa Syria dhidi ya Mayahudi.

Ndiyo, uko Gaza… Na Gaza inaangamizwa ukiwa huko.

Kinachosalia ni hadith ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kuhusu wale waliovuka mipaka:

«إِنَّ مِمَّا أَدْرَكَ النَّاسُ مِنْ كَلَامِ النُّبُوَّةِ إِذَا لَمْ تَسْتَحْيِ فَاصْنَعْ مَا شِئْتَ»

“Hakika miongoni mwa yaliyowafikia watu kutoka maneno ya Utume wa kwanza ni: Ikiwa huoni haya, basi fanya utakalo.” (Bukhari, Adab, 78).

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Muhammed Emin Yıldırım

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.