- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Harakati ya Taliban na Fursa ya Kusimamisha Khilafah
https://www.al-waie.org/archives/article/19755
(Imetafsiriwa)
Yousuf Arsalan - Afghanistan
Jarida la Al-Waie Toleo Na. 465
Mwaka wa Thelathini na Tisa,
Shawwal 1446 H sawia na Aprili 2025 M
Maisha haya ya dunia ni kama dimbwi la hasara, ambalo ni wale tu wanaojua kukamata fursa ndio wataokolewa. Kwa sababu hii, Siku ya Kiyama inaitwa “Siku ya Majuto,” kwa sababu watu wengi wamezama katika hasara ya kidunia, na wameshindwa kutumia fursa za thamani walizopewa katika maisha yao. Walipoteza kwa urahisi nyakati za dhahabu alizozitoa Mwenyezi Mungu (swt) kwa ajili ya mwamko na izza ya Umma.
Kinyume chake, waliotangulia katika wema watafurahia hadhi ya juu kesho Akhera, kwa sababu sifa yao mashuhuri ilikuwa ni kukamata fursa na kuziwekeza kwa wakati ufaao.
Fursa ni kama mawingu yanayopita ambayo hutoweka haraka bila kuonekana, au kama swara wa kasi ambaye ni vigumu kumkamata. Muumini lazima awe kama muindaji aliye macho, anayetafuta kila wakati kutumia fursa, na kuzitarajia kwa uangalifu. Hivyo basi, Mwenyezi Mungu (swt) anaweka mbele yetu, katika maisha yetu binafsi na ya kijamii, fursa za thamani mara kwa mara, za kufidia dhambi zetu, kuinua hadhi yetu ya kiroho, au kupata nasr (ushindi) na uongofu wa Mwenyezi Mungu (swt). Ni nzuri ilioje ibara, “Mola wako hukupa pumzi za hewa safi katika uhai wako, basi jidhihirishe kwazo. Huenda ikakufikia pumzi yake na kamwe hutahangaika baada ya hapo.”
Sisi ni Ummah tuliosifiwa na Mwenyezi Mungu (swt) kuwa ni umma bora ulioletwa kwa ajili ya wanadamu, kuwaongoza wanadamu kwa mujibu wa sheria za Uislamu na kuwaongoza kwenye haki. Mwenyezi Mungu (swt) ametutukuza kwa Uislamu, kwa sharti tushikamane nayo na tutimize Ba’yah (kiapo cha utiifu) yetu kwa Khalifa mmoja, kwa ajili ya kutekeleza kikamilifu ujumbe huu wa Risaalah wa walimwengu wote. Mwenyezi Mungu (swt) ametupa fursa hii adhimu ya kuishi katika ulimwengu huu, kuwa sehemu ya Umma wa al-Mustafa (saw), kuubeba ujumbe huu adhimu, na kujitahidi kuutimiza.
Hata hivyo, leo tunaishi katika zama ambazo Umma wa Kiislamu unaishi bila Khalifa, katika hali ya mfarakano na mgawanyiko. Tangu kuondolewa kwa Khilafah Uthmaniyya mwaka 1924 M, Umma umepata fursa kadhaa za kusimamisha Khilafah. Makundi ya kisiasa na kijeshi yanayodai kushikamana na Uislamu yameingia madarakani katika kipindi cha miaka mia moja hii iliyopita.
Hata hivyo, mara walipopata mamlaka, walikengeuka kutoka katika utekelezaji Uislamu, kama watawala wengine wote. Walijificha nyuma ya hoja kama vile maslahi, manufaa, uhalisia, au uwezo, na wakapotoka kutoka kwenye ujumbe wa Risaalah, wakijisalimisha kwa mfumo wa ulimwengu wa kisekula. Mwishowe, ima walianguka, au moto wa Uislamu ulizimwa nyoyoni mwao.
Makundi haya, kila yalipoingia madarakani, yalifeli kujifunza kutokana na yaliyopita na yalikosa kwa urahisi fursa zilizotolewa na Mungu.
Katikati ya haya, na katika karne iliyopita, fursa spesheli zilijitokeza kwa Waafghani kutetea Imani yao, na kufanya kazi kuelekea kusimamisha Khilafah. Hapo chini, tunahakiki kwa ufupi fursa tatu kuu katika historia ya kisasa ya Afghanistan ambapo Waafghani wangeweza kuchukua hatua kuelekea kusimamisha Khilafah lakini wakafeli kuzitumia.
Ingawa Afghanistan ilibakia kwa karne nyingi nje ya utawala rasmi wa Khilafah, uhusiano chanya daima umekuwepo kati ya ardhi hii na Khilafah. Wakati Khilafah Uthmaniyya, inayojulikana kama “mgonjwa wa Ulaya,” ilikuwa ikikabiliana na migogoro mingi, Afghanistan ilikuwa chini ya ushawishi wa Dola ya Uingereza. Sultan Abdul Hamid II, kwa umaizi mkubwa na juhudi, alijaribu kuinusuru Khilafah kutokana na hatima hii, lakini hatimaye akajikuta yuko peke yake. Alitoa wito jumla wa Jihad, akiwataka Waislamu wote duniani kuhifadhi kiini cha Khilafah.
Chini ya dhurufu hizi, Afghanistan ilijizuia kuchukua hatua yoyote, ikitoa visingizio vya kisiasa na kijiografia. Ajabu, watawala wa Afghanistan wa leo wanarudia hoja hizo hizo. Jambo la kushangaza ni kwamba, Bara Dogo la India pia lilikuwa chini ya udhibiti wa Waingereza na kijiografia mbali zaidi na ardhi ya kiini cha Khilafah. Hata hivyo, Waislamu katika Bara Dogo la India hawakusimama tuli. Walianzisha Tehreek-e-Khilafat (Harakati ya Khilafah) na kuchukua hatua muhimu, kifedha na kibinafsi, katika kuinusuru Khilafah Uthmaniyya.
Pindi Vita vya Kwanza vya Dunia vilipoanza, Khilafah Uthmaniyya iliamua kuingia vitani kwa ajili ya kuendelea kuwa hai na kujiunga na upande wa Wajerumani. Mnamo 1915, ujumbe wa pamoja wa Uthmaniyya na Ujerumani ulifika Kabul, kwa lengo la kumshawishi Amiri Habibullah Khan kutangaza Jihad dhidi ya Uingereza na Urusi ya Tsar. Hata hivyo, alijizuia kuchukua hatua, kwa kuwa alikuwa chini ya ushawishi na udhibiti wa Uingereza.
Ingawa Amiri Habibullah Khan, kama watawala wa leo, alitoa visingizio kama vile eneo la kijiografia na kutokuwa na uwezo, sababu halisi ya uamuzi wake ilikuwa nia yake ya kudumisha upendeleo wa Uingereza. Kwa hakika, Uingereza ilikuwa imemuahidi msaada wa kifedha wa rupia milioni 60 kwa badali ya kupitisha sera ya kutoegemea upande wowote, lakini bila shaka haikutimiza ahadi hii.
Wakati huo, Waislamu wa Bara Dogo la India walikuwa wakiweka matumaini yao kwa Waafghani, na makundi yao yalihamia Afghanistan, wakitumaini kwamba Waafghani wangewaunga mkono na kutangaza Jihad dhidi ya Uingereza. Kwa upande mwingine, Waislamu nchini Afghanistan, kinyume na amri za Amiri Habibullah Khan, walikuwa na mwelekeo wa kuinusuru Khilafah Uthmaniyya na Waislamu wa Bara Dogo la India. Waliuona uingilia kati wa Uingereza katika Vita vya Dunia kama wakati mwafaka wa kutafuta uhuru.
Hata hivyo, ili kuzuia hisia za Kiislamu miongoni mwa watu na kuzuia maasi yoyote, Habeebullah Khan aliwaendea maulamaa wa mahakama, akitumia ushawishi wao kuwatuliza watu. Maulamaa walitayarisha waraka uitwao "Utiifu kwa Amiri" na wakausambaza katika misikiti na kambi za kijeshi, wakiwataka watu kushikamana na sera za Amiri na kumuunga mkono.
Ujumbe kutoka Bara dogo la India, ukiongozwa na Ubaidullah Sindhi, ulifika Kabul, ambako waliweka makaazi kwa lengo la kuwasha moto wa matumaini ya Jihad na umoja wa Kiislamu. Wakati Amanullah Khan alipochukua mamlaka na vita vya uhuru wa Afghanistan dhidi ya Uingereza kuanza, wahamiaji kutoka Bara la India walicheza dori kubwa na walichangia kwa kiasi kikubwa katika mapambano.
Baada ya kushindwa kwa Uingereza na uhuru wa Afghanistan, matumaini mapya yalipamba moto katika nyoyo za Waislamu duniani kote. Wakati huo, ardhi pekee huru ya Kiislamu iliyobaki ilikuwa Afghanistan na Khilafah Uthmaniyya. Kadiri Afghanistan ilivyoweza kuishinda Uingereza, ambayo ilikuwa imezikalia kwa mabavu sehemu kubwa za ardhi za Waislamu na kuchangia katika kuporomoka kwa Khilafah Uthmaniyya, maslahi ya Waislamu nchini Afghanistan yaliongezeka na matumaini yao kwa hilo kama chanzo cha mwamko wa Kiislamu yaliongezeka.
Hii ilikuwa ni fursa ya kwanza ya kihistoria kwa Waafghani kusimamisha Khilafah. Waislamu wa Bara dogo la India walitarajia kwamba Jihad ya Afghanistan ingeendelea, na kwamba jeshi la Waislamu lingesonga kuelekea India iliyokaliwa kwa mabavu. Walimtaka hata Amanullah Khan kuchukua uongozi wa Waislamu, na kuchukua jukumu la kuhuisha Umma wa Kiislamu na kufikia umoja wake.
Hata hivyo, wahamiaji Waislamu kwa mara nyingine walivunjwa moyo, kwani hawakujua kwamba Amanullah Khan alikuwa amelelewa katika shule ya "kikatiba" na alikusudia kufuata sera za Mustafa Kemal. Hata hivyo, Amanullah Khan alisitasita kukataa moja kwa moja matakwa ya watu, hasa kama vile matakwa ndani ya Afghanistan ya kutangaza Khilafah yalipoongezeka.
Katika Loya Jirga Baghman uliofanyika mwaka 1924, kukomeshwa kwa uhusiano wa Khilafah na Afghanistan na Uturuki mpya zilikuwa miongoni mwa mada kuu za majadiliano. Maulamaa na Amanullah Khan walitumia siku nzima kujadili Khilafah, lakini bila kufikia hitimisho. Majadiliano yaliendelea hadi siku ya pili. Katika siku mbili hizi, Maulamaa walieleza kuondolewa kwa Khilafah kuwa ni tukio chungu na wakasisitiza kwamba uteuzi wa Khalifa ni faradhi ya Shariah. Baadhi ya maulamaa pia walimtaka Amanullah Khan ajitangaze kuwa Khalifa wa Waislamu.
Mulla Turkestani, katika taarifa fupi juu ya umuhimu wa Khilafah, alisema, “Ulamaa wa Kiislamu wa kila aina na wadhifa wanawaona watu wa Humayuni kuwa wanafaa na kustahiki Khilafah, na lazima mukubali nafasi hii adhimu. Hata hivyo, Amanullah Khan, kwa fikra na mwelekeo wake, alitaka kuanzisha dola ya kitaifa, na aliegemea mwelekeo wa kujihusisha na dola kubwa za dunia, ikiwemo Uingereza, ambayo alipigana nayo.
Amanullah Khan alikataa kidiplomasia ombi hili, akitoa visingizio kama vile maumbile yasiyo ya kikahika ya ombi hilo, kutoweza, na hata ubatili wa Khilafah. Akimjibu Mulla Turkestani, Amanullah alisema, “Mimi, kwa kuzingatia kauli zenu na za wengine, siwezi kubeba mzigo huu mzito, ambao nauona umejaa vikwazo visivyo kwisha, na sikubali kugawanyika kwa ulimwengu wa Uislamu. Kama nilivyosema, ni lazima tujadili manufaa na madhara ya kuwepo na kutokuwepo Khilafah. Baada ya hapo, kujitolea kwa msimamo wake kunategemea pekee maulamaa wa Uislamu.”
Makundi ya Kiislamu ambao wameingia madarakani hadi sasa, ambao wanajiona wao wenyewe kifikra na kisiasa wakipingana na mwelekeo wa Mustafa Kemal, Reza Shah, Amanullah Khan, Sharif Husayn, na masekula wengine na wanautaifa, kwa kweli, hawajaonyesha tofauti kubwa kutoka kwao. Wamefuata kwa kiasi kikubwa sera zile zile.
Sera za Amanullah Khan za kisekula, za kitaifa, za kivitendo, na zenye mwelekeo wa kiuchumi ziliwavunja moyo Waislamu, kama ambavyo sera hizo hizo zinavyoendelea kuwakatisha tamaa Waislamu leo chini ya viongozi wanaodai kuwa wa Kiislamu.
Misheni iliyokuwa imetafuta hifadhi nchini Afghanistan kutoka Bara Dogo la India hatua kwa hatua ilipoteza matumaini na hatimaye ikalazimika kuondoka Afghanistan na kuhamia kwengine. Kuvunjwa moyo huku kuliongezeka hasa wakati Amanullah Khan alipotia saini mikataba ya amani na Uingereza jijini Kabul na Rawalpindi, akiahidi kwamba Afghanistan haitakuwa tishio kwa Uingereza. Pia alieleza hamu yake ya kuanzisha mahusiano ya kisiasa na kiuchumi na Uingereza, jambo ambalo liliwavuruga zaidi Waislamu nchini India na nchi zengine za Kiislamu.
Fursa hii ilipotea, lakini Muungano wa Kisovieti ulipoikalia kwa mabavu Afghanistan, watu wa Afghanistan waliinuka kwa ujasiri usio na kifani, wakatangaza Jihad dhidi yake, na kukabiliana nao kwa uthabiti. Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu (swt) na kujitolea mhanga kwa watu, ushindi ulipatikana, na mujahidina wakapata dola yenye nguvu iliyo na zana za hali ya juu za kijeshi. Kwa mara nyingine tena, matumaini ya Waislamu duniani kote yalielekea Afghanistan.
Mujahidina, wahamiaji kutoka nchi mbalimbali za Kiislamu waliopigana pamoja na Waafghani, walitarajia kwamba siku moja Afghanistan itakuwa kitovu cha nguvu za kisiasa na Khilafah, ambayo itazikomboa nchi za Kiislamu kutoka mikono wa watawala wakandamizi.
Wajumbe kutoka makundi ya Kiislamu waliwasili nchini Afghanistan ili kuchukua fursa hii ya kihistoria ya kusimamisha Khilafah. Makundi ya kijihadi ya Waarabu na wasio Waarabu yalijawa na matumaini, hasa kwa vile baadhi ya mujahidina wa Afghanistan waliamini kuwa Khilafah ndio mfumo pekee wa Kiislamu. Mujahidina waliamini kwamba “Khilafah ni mwanga wa nuru ambayo kwayo Waislamu wanaizunguka kama vipepeo.”
Hata hivyo, mujahidina wa Afghanistan waliamua kuunda dola ya kitaifa na wakazama katika ulevi wa madaraka. Mizozo ya ndani na mapambano ya ushawishi yaliwaongoza kukengeuka kutoka kwa njia kuu, na kusababisha maangamivu yao wenyewe.
Matokeo yake, sio tu kwamba wahamiaji Waislamu wa Afghanistan na mujahidina walivunjwa moyo, bali wengi walirudi nyumbani, huku wengine wakihamia nchi zengine.
Hii ilikuwa ni mara ya pili kwa Waafghani kukosa fursa kubwa ya kihistoria ya kusimamisha Khilafah, baada ya kuanguka kwa himaya nyengine.
Wakati huu, sisi ni kizazi kinachoshuhudia kushindwa kwa NATO na kuibuka kwa fursa ya tatu iliyotolewa na Mwenyezi Mungu ya kusimamisha Khilafah Rashida ya Pili nchini Afghanistan na eneo hilo. Kushindwa kwa Amerika na NATO katika ardhi hii kumezua matumaini mapya kwa Waislamu duniani kote kwamba Afghanistan inaweza kuchukua fursa hii ya dhahabu na kutorudia makosa ya zamani.
Jambo muhimu ni kwamba fursa hii ya kimungu ilikuja chini ya dhurufu za kipekee. Kwa upande mmoja, NATO ilishindwa nchni Afghanistan, na kwa upande mwingine, Magharibi ilishughulishwa sana na vita vya Ukraine, na sera ya kuidhibiti China.
Hali hii inawakilisha fursa ya kipekee kwa Waislamu nchini Afghanistan kuchukua fursa ya dhurufu hizi na kuchukua hatua ya kihistoria kuelekea kusimamisha Khilafah Rashida, kwa kutumia fursa ya kujishughulisha kwa maadui zao na mizozo yao wenyewe.
Sasa, mateso ya Waislamu yanazidi kwa sababu ya vita dhidi ya Gaza, na wito unatolewa kutoka katika Ulimwengu wote wa Kiislamu kwa Mujahidina nchini Afghanistan kujitokeza kuwasaidia kaka na dada zao. Kwa hivyo swali la msingi linazuka, je, watawala wa Afghanistan wataweza kunyakua fursa hii ya kihistoria, au watafanya kama walivyofanya watangulizi wao na kujiunga na safu ya wale wanaouma vidole vyao kwa majuto?
Historia ni kitabu kilichojaa mafunzo. Amanullah Khan, ambaye aliitumia vibaya fursa hii aliyopewa na Mwenyezi Mungu na kuchagua kutimiza agano lake na Uingereza badala ya kutimiza mapatano yake na Mwenyezi Mungu (swt), hakuweza kufikiria kwamba mtu asiye maarufu kama Amiri Habibullah Kalakani angeweza kuhujumu utawala wake.
Je, hatima ya mujahidina wa Afghanistan ambao walipigana dhidi ya Wasovieti na kisha wakakimbilia hifadhi katika serikali ya kitaifa, ila tu kuzama katika mapenzi wa kidunia, mbele ya macho yetu?
Sasa je, watawala walioingia madarakani nchini Afghanistan, Syria na nchi nyingine za Kiislamu chini ya bendera ya Uislamu, wataendelea kuwasilisha hoja zilezile za maadui wa Uislamu, wakihalalisha sera zao zisizo za Kiislamu, ingawa wameona matokeo yake kwa waliowatangulia?
Sasa, katika fursa hii ya tatu ya kihistoria, Hizb ut Tahrir inatoa wito kwa uwazi kabisa kwa watawala wa Afghanistan kusimamisha Khilafah Rashidah ya Pili. Hata hivyo, jibu lao litakuwa nini?
Je! tutaona tena ukimbiaji fursa za kimungu, au je, wakati huu kutakuwa na jibu la kweli kwa wito wa historia na wajibu?
Mlango wa fursa umebaki wazi, na Waislamu duniani kote, hususan Mujahidina wahamiaji waliopigana bega kwa bega na Waafghani, wamekuwa wakiitarajia siku hii ambapo Dini ya Mwenyezi Mungu (swt) itakapotukuzwa, waliodhulumiwa watapata ushindi, na Khilafah itasimamishwa, ikiunganisha sehemu zilizotawanyika za Ummah na kuregesha izza yake.
Furaha iko katika ukweli kwamba mlango huu bado uko wazi. Fursa ya mujahidina wa leo ni kuwa answar wa leo, kwa kutoa nusrah (msaada wa silaha) kwa Hizb ut Tahrir. Walakini, mlango huu hautabaki wazi milele. Yeyote aliye na mlango wa kheri, uliofunguliwa kwa ajili yao, lazima ainuke mara moja na atumie fursa hiyo, kwa sababu hawajui ni lini utafungwa. Wasipofanya hivyo watakuwa miongoni mwa wenye kujuta Siku ya Kiyama.
Kwa hiyo, tunautahadharisha Ummah na viongozi wake dhidi ya uzembe na upotevu wa fursa hizi adhimu, kama anavyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
[وَأَنذِرْهُمْ يَوْمَ الْحَسْرَةِ إِذْ قُضِيَ الْأَمْرُ وَهُمْ فِي غَفْلَةٍ وَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ]
“Na waonye siku ya majuto itapo katwa amri. Nao wamo katika ghafla, wala hawaamini.” [Surah Maryam:39]. Fursa iko mbele yetu, lakini lazima tutambue kwamba mlango huu hautabaki wazi milele, na wale wanaosita leo watajuta kesho.