Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

Sudan: Janga la Karne Lililofichika Machoni mwa Ulimwengu
(Imetafsiriwa)

Dola ya Kiislamu, mlinzi wa watu wake, haipo. Waislamu wameishi katika taabu, mateso, na majanga duniani kote. Sudan hivi sasa inakabiliwa na moja ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu katika historia ya kisasa kutokana na mapigano ya umwagaji damu ambayo yamekuwa yakiendelea kwa miaka miwili kati ya jeshi na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), na kusababisha maafa ya kutisha ambayo hakuna anayezungumza au kujaribu kuzuia. Huu ni mzozo uliosahaulika ambao vyombo vya habari haviupi mwanga, na ambao maelezo yake hayafichuliwi na dola yoyote au hata taasisi zake.

Raia wanakabiliwa na ukiukwaji mkubwa wa haki, ikiwemo mauaji ya watu wengi, kulazimishwa kuhama makaazi yao na kutafuta hifadhi, njaa, magonjwa, unyanyasaji wa kijinsia na maafa mengine, na hakuna mtu wa kufuatilia au kuwajibisha!

Huku ukatili ukifanywa na pande zote mbili zinazopigana, makadirio yanaonyesha idadi ya kushtua ya waliokufa na waliojeruhiwa, hasa miongoni mwa wanawake, watoto, na wazee. Idadi ya vifo inakadiriwa kuwa angalau watu 150,000, ikiwemo zaidi ya 60,000 katika jimbo la Khartoum pekee, katika pindi cha miezi 14 ya kwanza ya vita.

Idadi ya waliojeruhiwa imezidi 70,000, huku kukiwa na ugumu mkubwa wa kupata huduma za matibabu kutokana na kuporomoka kwa mfumo wa afya, ambapo asilimia 70-80 ya vituo vya afya havina huduma, na kuenea kwa magonjwa ya kipindupindu, ukambi na kuhara. Elimu nayo imeporomoka; karibu watoto milioni 20 nchini Sudan kwa sasa hawako shuleni.

Maeneo mengi yalishuhudia mauaji ya kutisha, mauaji ya kinyama, utekaji nyara, na mateso, ikiwemo watoto. Haya yalijumuisha mauaji ya Wad al-Nura, al-Hilaliya, Jalqani, al-Sariha, Tamboul, kambi ya Zamzam, vijiji vya Darfur Kaskazini, al-Geneina, Ardamata, na vijiji katika Jimbo la White Nile katikati mwa Sudan. Mauaji haya yalisababisha vifo vya maelfu ya raia na mamia ya maelfu kuyahama makaazi yao. Hii ikiwa ni pamoja na uhalifu wa unyanyasaji wa kingono na ubakaji wa magenge dhidi ya wanawake, wasichana, na hata watoto.

Mapigano haya yamewahamisha makaazi zaidi ya watu milioni 14, kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji. Kati ya hao, zaidi ya milioni 11 ni wakimbizi wa ndani kwa ndani nchini Sudan, na zaidi ya milioni 3 ni wakimbizi ambao wamekimbilia nchi jirani kama vile Misri, Ethiopia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini, Chad na hata Jordan.

Watoto wanawakilisha 53% ya wakimbizi wa ndani, na kuifanya Sudan kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi wa ndani ulimwenguni. Watu waliokimbia makaazi yao ni takriban theluthi moja ya wakaazi wa Sudan wenye takriban milioni 50. Kambi za wakimbizi hazina huduma za kimsingi, na zinakabiliwa na uhaba wa chakula, maji safi, na huduma za afya. Kambi hizi pia zinakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara, na kuzidisha mateso ya waliokimbia makaazi yao.

Haya yote yamesababisha mgogoro mkubwa wa chakula, hasa kutokana na pande zote mbili kutumia njaa kama silaha ya vita kwa kuzuia chakula kuingia katika maeneo wanayodhibiti. Takriban watu milioni 25 – karibu nusu ya watu – wanahitaji msaada wa chakula, hasa katika kambi za wakimbizi. Mamia ya maelfu ya watoto wanakabiliwa na utapiamlo mkali, na idadi kubwa yao iko katika hatari ya kufa. Ripoti zinaonyesha kuwa takriban watoto milioni 3.7 nchini Sudan wanakabiliwa na utapiamlo. Idadi hii inatarajiwa kuongezeka iwapo hali itaendelea, na takriban watoto 220,000 wanaokabiliwa na utapiamlo mkali huenda wakafariki.

Hii ina maana kwamba Sudan, ambayo ilionekana kuwa kikapu cha chakula duniani kutokana na wingi wa ardhi ya kilimo, maji, na mifugo, sasa ina wakaazi wanaokabiliwa na njaa, umaskini, magonjwa na kuhama makaazi yao. Hivi sasa inakabiliwa na maafa makubwa zaidi ya kibinadamu katika nyanja zote kutokana na vita vilivyolaaniwa kati ya jeshi na Vikosi vya Msaada wa Haraka, ili kuendelea kutimiza matamanio ya bwana wao, Amerika, nchini Sudan na utajiri wake, ambayo gharama yake kubwa hulipwa pekee na watu wa Sudan wanaoteseka.

Mapambano haya yataendelea nchini Sudan na nchi nyingine za Kiislamu maadamu matamanio ya kikoloni yanaendelea na watawala Ruwaibidha (wajinga na watepetevu) wanawakandamiza. Kwa hivyo, Enyi watu, fanyeni kazi ya kuwapindua na kusimamisha Khilafah Rashida ya pili kwa njia ya Utume ili Sudan na nchi zote za Kiislamu ziweze kukombolewa kutoka katika mshiko wa ukoloni kwa maumbo na mbinu zake zote. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[ذَلِكَ بِأَنَّ اللهَ لَمْ يَكُ مُغَيِّراً نِّعْمَةً أَنْعَمَهَا عَلَى قَوْمٍ حَتَّى يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ]

“Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa neema alizo waneemesha watu, mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao. Na hakika Mwwnyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.” [Al-Anfal: 53].

Na kama alivyosimulia Ibn Majah kutoka kwa Abdullah bin Omar, Mwenyezi Mungu awe radhi nao wote wawili, ambaye amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alitujia na kusema:

«يَا مَعْشَرَ الْمُهَاجِرِينَ: خَمْسٌ إِذَا ابْتُلِيتُمْ بِهِنَّ، وَأَعُوذُ بِاللهِ أَنْ تُدْرِكُوهُنَّ؛ لَمْ تَظْهَرْ الْفَاحِشَةُ فِي قَوْمٍ قَطُّ حَتَّى يُعْلِنُوا بِهَا إِلَّا فَشَا فِيهِمْ الطَّاعُونُ وَالْأَوْجَاعُ الَّتِي لَمْ تَكُنْ مَضَتْ فِي أَسْلَافِهِمْ الَّذِينَ مَضَوْا، وَلَمْ يَنْقُصُوا الْمِكْيَالَ وَالْمِيزَانَ إِلَّا أُخِذُوا بِالسِّنِينَ وَشِدَّةِ الْمَئُونَةِ وَجَوْرِ السُّلْطَانِ عَلَيْهِمْ، وَلَمْ يَمْنَعُوا زَكَاةَ أَمْوَالِهِمْ إِلَّا مُنِعُوا الْقَطْرَ مِنَ السَّمَاءِ، وَلَوْلَا الْبَهَائِمُ لَمْ يُمْطَرُوا، وَلَمْ يَنْقُضُوا عَهْدَ اللهِ وَعَهْدَ رَسُولِهِ إِلَّا سَلَّطَ اللهُ عَلَيْهِمْ عَدُوّاً مِنْ غَيْرِهِمْ فَأَخَذُوا بَعْضَ مَا فِي أَيْدِيهِمْ، وَمَا لَمْ تَحْكُمْ أَئِمَّتُهُمْ بِكِتَابِ اللهِ وَيَتَخَيَّرُوا مِمَّا أَنْزَلَ اللهُ إِلَّا جَعَلَ اللهُ بَأْسَهُمْ بَيْنَهُمْ».

“Enyi Muhajirun kuna mambo matano mtatahiniwa nayo, na najikinga kwa Mwenyezi Mungu msije mkawa hai na kuyaona: Uasherati hautadhihiri kamwe katika watu kiasi kwamba wanaufanya waziwazi, isipokuwa tauni na maradhi ambayo hayakujulikana miongoni mwa waliotangulia yataenea miongoni mwao. Hawatadanganya katika vipimo na mizani isipokuwa watasibiwa na miaka ya ukame na njaa, na ugumu wa maisha, na udhalimu wa watawala wao. Na hawatazuia kutoa zaka ya mali zao, isipokuwa mvua itazuiliwa kutoka mbinguni, na lau kuwa si wanyama, mvua isingewanyeshea. Na hawatavunja ahadi yao na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, isipokuwa Mwenyezi Mungu atawapa uwezo maadui zao kuwashinda na kuchukua baadhi ya yale yaliyomo mikononi mwao. Na viongozi wao  hawatatawala kwa mujibu wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na wakachagua miongoni mwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu atajaaliya mgongano baina yao.”

Hii, wallahi, imekuwa ndiyo hali yetu na hali yetu katika nchi za Kiislamu tangu kutoweka kwa jua la Khilafah na mchungaji na kiongozi anayetawala kwa Sharia na Dini ya Mwenyezi Mungu.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Muslimah Ash-Shami (Umm Suhaib)

#أزمة_السودان

#SudanCrisis

#SudanKrizi

#SoudanCrise

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.