Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali

Mkutano kati ya Trump na Putin huko Alaska
(Imetafsiriwa)

Swali:

Rais Trump wa Marekani na Rais wa Urusi Putin walifanya mkutano huko Alaska mnamo tarehe 16/8/2025. Je, walifikia makubaliano kuhusu masuala muhimu? Je, mkutano huu ulikuwa na athari gani katika mahusiano kati ya nchi hizi mbili? Kuhusu Ukraine? Na kimataifa kuhusu Ulaya na China?

Jibu:

Ili kufafanua majibu ya maswali hayo ya juu, tunahakiki mambo yafuatayo:

1- Uhusiano kati ya Amerika na Urusi umebadilika katika miongo mitatu iliyopita kutoka kwa uhusiano kati ya dola mbili kuu kudhibiti hatima ya ulimwengu kabla ya kuanguka kwa Muungano wa Kisovieti mnamo 1991, hadi kujiondoa kwa Urusi kwenye uwanja wa kimataifa na kujiondoa yenyewe kwenye muungano huo na kubakia nchi kipeke yake, huku Amerika ikifuatilia kina cha mporomoko wa Urusi na majaribio yake ya kunyakua maeneo ya ushawishi ya enzi ya Usovieti. Kisha, kwa majaribio ya Rais wa Urusi Putin kuirejesha Urusi kama dola kuu yenye hadhi ya kimataifa, na Marekani kulikataa hili. Katika ishara ya kina cha mzozo kati ya malengo ya nchi hizo mbili, vita vilizuka nchini Ukraine mnamo 2022, ambapo Urusi ilijaribu kunyanyua msimamo wake wa kimataifa kwa nguvu, na Amerika ikataka, kupitia uungaji mkono wake kwa Ukraine, kuiondoa Urusi kwenye orodha ya dola kuu. Hali hii ilibakia kuwa hivyo hadi mwisho wa utawala wa Biden. Wakati Trump alipokuwa rais wa Marekani tena, alianza kuelekeza dira ya Amerika dhidi ya China, na akatangaza hamu yake ya kupunguza mvutano na Urusi. Alisema alikuwa na uwezo wa kumaliza vita nchini Ukraine ndani ya masaa 24, na kwamba vita hivi havikuwa vita vyake, bali vita vya Biden. Kwa hivyo, chini ya Trump, Amerika ilianza kubadilisha uhusiano wake na Urusi. Hili lilidhihirika kutokana na matusi ya mara kwa mara ya Rais Trump dhidi ya Rais wa Ukraine Zelenskyy, ukosoaji wake mkali wa uungwaji mkono wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine, na kutaka nchi za Ulaya zichukue majukumu yao ya kifedha na kijeshi nchini Ukraine.

2- Vita vya Ukraine vimedhoofisha hadhi ya kimataifa ya Urusi. Jeshi lake limethibitisha kutoweza kufikia malengo ya haraka, yenye thamani ya juu nchini Ukraine. Karibu nusu ya meli zake za nevi ziliharibiwa katika Bahari Nyeusi, kambi yake ya kimkakati ndani kabisa ya Urusi ilishambuliwa, na imepoteza vitu muhimu kwa vikosi vyake vya ardhini, vikiwemo vifaa na majenerali. Hata hivyo, haijashindwa na imebaki na uwezo wa kufanya maendeleo ndani ya Ukraine, hata kama inasifiwa kuwa mtambao wa mchwa. Hata hivyo, Urusi ambayo imejikuta ikikabiliana na uwezo wa kijeshi wa NATO, kana kwamba inapigana na nchi za NATO, imeonyesha kuchanganyikiwa, wakati mwingine ikitoa kauli na maandalizi ya nyuklia. Hii ni hatari sana na sivyo Amerika inavyotaka. Kwa maana nyengine, vita vya Ukraine vimeangazia hatari za kuongezeka kwa vita vya nyuklia. Vita vya Ukraine vimemfanya rais wa Urusi Putin kuimarisha ushirikiano wake wa kimkakati na China. Ingawa hali hii ilitarajiwa kutoka Amerika, na licha ya China kutoijibu Urusi kwa joto lile lile, isije ikapoteza uhusiano wake muhimu wa kibiashara na Amerika na Ulaya, kugawanyika upya kwa ulimwengu katika kile kinachofanana na kambi mbili ni jambo la mwisho ambalo Amerika inalitaka. Haitaki kabisa nguvu za kiuchumi za China ziongezee nguvu za kijeshi za Urusi katika kambi moja.

3- Hofu ya Urusi ya kushindwa kimkakati ambayo Amerika inapanga nchini Ukraine imeichochea kuongeza makombora na silaha zake za nyuklia. Makubaliano ya nyuklia na Marekani ni ya kiwango cha chini kufuatia kujiondoa kwa Amerika mnamo 2019 kutoka kwa Mkataba wa Vikosi vya Nyuklia vya Masafa ya Kati. Mbali na Urusi kuanzisha makombora ya hypersonic katika vita vyake nchini Ukraine, pia ilianzisha kombora la Oreshnik lenye uharibifu mkubwa mnamo 2024. Hatimaye, muda mfupi kabla ya mkutano wa Putin na Trump, Urusi ilitangaza majaribio ambayo Amerika ilikuwa na ufahamu wa maandalizi ya Urusi kwa ajili yake, ya makombora ya nyuklia yenye injini za nyuklia pia, ikimaanisha masafa yasiyo na mipaka na kasi isiyo na kikomo. Mbali na hatari inayoiweka kwa Marekani na ukweli kwamba ingeondoa ngao yake ya makombora ambayo imekuwa ikithaminiwa sana, ambayo imetumia mabilioni ya pesa juu yake, pia inathibitisha kwa Amerika kwamba Urusi inafuata mbio mpya za kimkakati za kijeshi, bila kujali gharama ya uchumi wake. Hili linahitaji Amerika kufikia makubaliano na Urusi kusitisha kusonga mbele na kuepusha mbio za kijeshi mithili ya Vita Baridi.

4- Urusi ilikabiliwa na uwezekano wa kushindwa kijeshi nchini Ukraine. Picha yake ya kijeshi kama dola kuu ilichanwa na haikuweza kushinda jeshi la Ukraine. Vita hivyo vilikuwa vya kurudi nyuma na mbele, ikimaanisha kwamba Urusi ilipoteza manufaa yake ya kimaamuzi, ambayo iliudhuru msimamo wake wa kimataifa. Mbali na udhaifu wake wa kijeshi ulioonekana wazi nchini Ukraine, iliangukia chini ya kifurushi kikubwa cha vikwazo vya Magharibi ambavyo karibu kuifikisha kwenye ukingo wa kujiondoa katika uchumi wa dunia na kulazimisha kutengwa kukubwa kimataifa juu yake. Rais wa Urusi hakuweza hata kutembea kwa uhuru nje ya nchi kutokana na hati za kukamatwa kwake zilizotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu. Kwa hivyo, Urusi ilipeleka uwezo wake wote wa kiuchumi na kijeshi ili kuzuia mzuka wa kushindwa kimkakati katika vita vya Ukraine. Uchumi wake ukawa uchumi wa vita. Iliamini kwamba msimamo wake wa kimataifa uliamuliwa na vita vya Ukraine. Hata hivyo, hofu ya kushindwa haikuondoka, na hofu yake kubwa ilikuwa kwamba mambo yangeongezeka kuelekea kuingilia kati kwa NATO na kukabiliana nayo moja kwa moja. Haina uwezo wa kufanya hivyo isipokuwa itatumia zana zake za nyuklia, lakini kutumia zana hizi ni hatari na hatari sana. Wakati Rais Trump wa Marekani alipokuja na kuanza kuisifia Urusi na kumsifu rais wake, Urusi ilipumua, kwani hii iliwakilisha kuhama kwa Marekani kutoka kwenye mipango yake ya kushindwa kimkakati kwa Urusi. Huenda Urusi ilizingatia kukubali ofa za Trump kwa vile zilikuwa za kudhibiti kumalizika kwake, lakini inatazama mlango aliofungua Trump kwa ajili ya kuregea katika ulingo wa kimataifa, na iko ukingoni ikihofia unaweza kufungika wakati inapotaka kuingia humo.

5- Wakati Amerika iliposhuhudia kusitasita na kukataa kwa Urusi kusitisha vita, na sauti zikaongezeka katika nchi za Magharibi kwamba Putin alikuwa anatumia mbinu ya hivi karibuni ya Trump na nia ya kusitisha vita nchini Ukraine, rais wa Marekani alitangaza makataa ya siku 50 kwa Urusi kusitisha vita nchini Ukraine. Licha ya kukerwa sana kwa Urusi na tarehe hii ya mwisho na ombi lake la ufafanuzi, iliendelea kuakhirisha ndani ya tarehe hii ya mwisho, ikitaka kuitumia hadi mwisho. Hii ilimfanya rais wa Marekani kutishia kuchukua mgeuko, yaani, kufunga mlango na kurejea katika misimamo ya utawala wa Biden. Alitangaza kwamba kipindi hiki kitafupishwa hadi siku 10 tu, ambazo Urusi iliona, kupitia Naibu Mshauri wa Usalama wa Kitaifa na Rais wa zamani Medvedev, kama hatua ya kuelekea kwenye vita. Medvedev aliikumbusha Amerika juu ya “mkono wa nyuklia wa siku ya mwisho” wa Urusi, na rais wa Amerika alibadilishana maneno naye, ambaye alimhimiza kuwa mwangalifu kwamba anaingia katika eneo hatari sana. Kwa tishio hili la Marekani la kuchukua mgeuko na kuregea kuiunga mkono Ukraine na kuiwekea Urusi vikwazo vikali zaidi, ikiwa ni pamoja na wale wote wanaonunua mafuta kutoka humo, yaani China hasa, saa ziliziyoyoma jijini Moscow kwamba ilibidi uamuzi ufanywe.

6- Urusi kwa hivyo ilihisi lazima ifanye makubaliano haraka na Amerika. Haitaki kuregea kwa kasi ya uungaji mkono wa Marekani kwa Ukraine, jambo ambalo lingeweka mkazo zaidi na kupoteza fursa iliyotolewa na Rais Trump kuvunja kutengwa kwake kimataifa. Zaidi ya hayo, Urusi ina shaka kuhusu China. Ikiwa China ingepewa chaguo kati ya kufaidika na mafuta ya bei nafuu ya Urusi na mahusiano yake ya kibiashara na Amerika, bila shaka ingechagua la pili, kutokana na faida zake nyingi. Zaidi ya hayo, ofa ya amani ya Trump inaipatia Urusi kile inachotaka kutokana na makubaliano na Marekani pekee, sawa na Mkutano wa Yalta mwaka wa 1945. Haitaki kuhusisha pande zengine za Ulaya au Ukraine, bali inataka makubaliano na Marekani ambayo yatawasilishwa kwa pande nyingine kama fait accompli (kuyakubali bila khiyari). Hivyo, Urusi ilichukua hatua ya kuomba kukutana na mjumbe wa Rais Trump wa Marekani, Witkoff, ili kuondoa wazo la makataa iliyopewa Urusi. Kwa hakika hii inaihitaji kuacha baadhi ya matakwa yake. Katika mkesha wa mkutano wa kilele kati ya marais hao wawili na katika kipindi kifupi cha maandalizi, pande zote mbili zilionyesha dalili za kutaka mkutano huu, na Trump kweli alijibu ombi la Urusi la kutuma mjumbe wake maalum, Witkoff, jijini Moscow. Trump alizungumza juu ya fursa na kubadilishana ardhi na mipaka kati ya Urusi na Ukraine, na Urusi ilizungumza juu ya ikhlasi ya Amerika: “Putin alisema kuwa Moscow inajitahidi kuweka mazingira ya amani, na kwamba Marekani “inafanya juhudi za dhati” kutatua hali kuhusiana na Ukraine. Putin alisisitiza umuhimu wa kufikia makubaliano na Washington juu ya kupunguza silaha za kimkakati za mashambulizi.” (Al Jazeera Net, 14/8/2025). Urusi ilikubali mkutano wa kilele unaofanyika Alaska, yaani Marekani, ili kumtuliza Trump: “Trump anaamini kwamba uamuzi wa Rais wa Urusi Vladimir Putin kusafiri hadi Alaska kukutana naye ni “kitendo cha heshima kubwa.” (RT, 12/8/2025)

7- Lakini kwa upande mwengine, Amerika, huku ikiwa imeshuhudia uakhirishaji wa Urusi kwa miezi kadhaa baada ya Trump kufika Ikulu ya White House, haikutaka mkutano huu wa kilele uwe bila makubaliano na Urusi. Trump alisema kuwa mkutano huu ulikuwa wa “kuvunjari,” na kwamba angejua kutoka dakika za kwanza za mkutano huo ikiwa Putin alikuwa na nia ya kumaliza vita vya Ukraine au la. Alionya juu ya kufeli kwa mkutano huo, na kuweka uwezekano wa 25% wa kufeli kwake, na kuitishia Urusi kwa matokeo mabaya: (Rais wa Marekani Donald Trump alimtishia mwenzake wa Urusi Vladimir Putin mnamo Jumatano kwa “matokeo makubwa” endapo atazuia jitihada za kufikia amani ya Ukraine, na kutishia uwezekano wa kuweka vikwazo vya kiuchumi ikiwa mkutano wao uliopangwa kufanyika Ijumaa huko Alaska hautafanikiwa kufikia matokeo ya kushikika. Trump alieleza kuwa mkutano na rais Putin utakuwa ni “maandalizi” ya mkutano wa pili ambao ungemjumuisha rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, akiashiria kuwa kufanyika kwake kunategemea matokeo ya mkutano wa Alaska. (Arab 48, 14/8/2025)

Rais wa Marekani Donald Trump kisha akautaja mkutano wake wa kilele na Vladimir Putin kuwa “wa hali ya juu” kabla ya kuelekea Anchorage, Alaska, kufanya mkutano wao wa kwanza tangu miaka saba iliyopita. Trump alielezea hamu yake ya kuona usitishaji mapigano “haraka sana.” (Independent Arabia,, 15/8/2025). Trump alisema angeharakisha kurudi kutoka Alaska hadi Washington ikiwa Putin hayuko makini. (Rais wa Marekani Donald Trump aliwasili katika Kambi ya Jeshi la Wanahewa ya Elmendorf huko Anchorage, Alaska, mnamo Ijumaa. Trump alisema kwamba ikiwa mkutano wa kilele na Rais wa Urusi Vladimir Putin utaenda vibaya, ataondoka. (CNN Arabic, 15/8/2025)). Kauli hii ya kuondoka kwenye mkutano inabeba aina fulani ya matusi kwa Rais Putin, ambaye alikuja kukutana na Trump nchini Amerika!

8- Taarifa hizi zote zinaweka shinikizo kwa Urusi kufanya makubaliano, kwani anaitishia kwa matokeo mabaya, vikwazo, na kujiondoa kwenye mkutano. Hii ina maana kwamba mkutano kati yao haukuwa na uwiano kama ilivyokuwa mikutano muhimu kati ya viongozi wa Usovieti na Marekani huko nyuma. Huu sio mkutano wa dola kuu mmili, na haujapanda hata daraja ya mikutano ya kilele ya Amerika na China. Inaimarisha kiburi cha Amerika na matakwa yake ya kujisalimisha kwa Urusi, pamoja na kushuka kwa hadhi ya Urusi mpya, ambayo ilikubali masharti haya yote ya Amerika, makataa na vitisho. Rais wake alisafiri hadi Amerika kufanya mkutano na Trump badala ya kufanywa katika nchi ya tatu. Pengine hatua inayokinzana na itifaki ni Rais Putin wa Urusi kukubali ombi la rais wa Marekani la kupanda naye gari lake binafsi, licha ya uwepo wa gari la Putin ambalo huambatana naye katika mikutano yake yote ya kimataifa, ni ushahidi wa kujisalimisha kwa Urusi kwa matakwa yake ya kuwa na uhusiano wa harara na Trump ili kupunguza hasara zake za kimkakati. Kinachothibitisha hilo ni kwamba licha ya mpasuko mkubwa wa uhusiano kati ya Marekani na Urusi uliowekwa na utawala wa Biden, rais huyo wa Urusi alikuwa na nia ya kumshawishi Trump. Yuri Ushakov, msaidizi wa rais wa Urusi alisema: “Ushirikiano kati ya Urusi na Marekani una uwezo mkubwa sana ambao haujatumiwa. Alibainisha kuwa ujumbe wa Urusi utajumuisha Msaidizi wa Rais Yuri Ushakov, Waziri wa Mambo ya Nje Sergey Lavrov, Waziri wa Fedha Anton Siluanov, na Mwenyekiti wa Mfuko wa Uwekezaji wa Moja kwa Moja wa Urusi Kirill Dmitriev.” (RT, 14/8/2025). Hiki ni kiashiria cha udhaifu wa Urusi ambao Marekani ina uhakika wa kuukabili. Labda kauli za Rais Putin wa Urusi baada ya mkutano huo zinaonyesha udhaifu huu na kina cha wasi wasi wa Urusi kuhusu kuendelea kwa mvutano katika mahusiano kati ya nchi hizo mbili. Rais wa Urusi alianza hotuba yake katika mkutano na waandishi wa habari kwa kukiri kuzorota kwa uhusiano kati ya Marekani na Urusi katika miaka ya hivi karibuni. Alisema, “Kama inavyojulikana, mikutano ya kilele ya Urusi na Amerika haijafanyika kwa zaidi ya miaka minne. Huu ni muda mrefu. Kipindi cha nyuma kilikuwa kigumu sana kwa uhusiano wa pande hizi mbili. Na, tuseme ukweli, umeshuka hadi hatua ya chini kabisa tangu Vita Baridi. Na hii sio vizuri kwa nchi zetu, au ulimwengu kwa ujumla.” Aliongeza: “Ni wazi, sasa au baadaye, ni muhimu kurekebisha hali hiyo, kutoka kwa makabiliano hadi mazungumzo. Na katika suala hili, mkutano wa kibinafsi wa marais wa dola hizi mbili ulikuwa umechelewa sana.” Putin alisema: “Mazungumzo yalifanyika katika mazingira ya heshima, yenye kujenga, na kuheshimiana na yalikuwa ya kina na yenye manufaa.” (Reuters, CNN Arabic, 16/8/2025)

9- Kumalizia, kwa kuchunguza kwa makini mwenendo wa mkutano kati ya Trump na Putin na uangaziaji wa vyombo vya habari, inaweza kusemwa kwamba mambo yafuatayo yalizungumziwa katika mkutano wao:

a- Ukraine: Hili ndilo suala kuu zaidi, ingawa sio suala pekee, lakini ndilo maarufu na moto zaidi. Licha ya uthabiti wa matakwa ya usalama ya Urusi, yaani, Ukraine iondolewe katika NATO na isimiliki jeshi imara linaloitishia Urusi, makubaliano ya wazi yalibainishwa katika mkutano huo. Kipengee kimoja cha makubaliano haya kilikuwa ahadi ya mustakabali ya Urusi kutoishambulia Ukraine.” (Putin alisisitiza kwamba anakubaliana na haja ya kudhamini usalama wa Ukraine, akisema: “Nakubaliana na Rasi Trump, kama alivyosema leo, kwamba kimaumbile, usalama wa Ukraine unapaswa kuhakikishwa vilevile. Kimaumbie, tumejitayarisha kulifanyia kazi hilo.” Aliongeza: “Ningependa kutaraji kuwa makubaliano haya ambayo tumeyafikia kwa pamoja yatatusaidiwa kulileta karibu lengo hilo na yatatoa njia ya amani nchini Ukraine.” (CBS, CNN Arabic, 16/8/2025)). Kinachothibitisha pia uwepo wa makubaliano ni kwamba Rais wa Marekani aliupa mkutano wake na Putin alama 10 kwa 10. (Sky News, 16/8/2025). Amerika inapoza eneo la vita nchini Ukraine kwa maandalizi ya kusitisha mapigano. Hii inahitaji ahadi ya Marekani kupunguza hatua kwa hatua uungaji mkono wa kijeshi wa Marekani na Magharibi kwa jeshi la Ukraine, kisha kutangaza usitishaji mapigano, ambao unaweza kuja kupitia mkutano wa kilele kati ya marais hao wawili na Rais wa Ukraine Zelenskyy ndani ya wiki chache. Kisha kuendelea na suluhisho nchini Ukraine polepole, labda katika kipindi cha miaka kadhaa. Kwa maana nyengine, Amerika inaakhirisha suluhisho la mwisho na inataka usitishaji wa haraka wa mapigano. Suluhisho la mwisho lazima liwe kwa miaka mingi, wakati ambapo Amerika itailazimisha Ukraine kupeana eneo na mipaka sawa na makubaliano ambayo Urusi itafanya kwa Amerika katika maswala mengine. Hii ni kana kwamba inaifanya Urusi idondoke mate kwa kutambua kwake mipaka ya udhibiti wa Urusi nchini Ukraine, kwa masharti ambayo Urusi inapaswa kuyatimiza na kuiridhisha Marekani.

b- Kurekebisha upya mahusiano ya Marekani na Urusi: Ingawa mchakato huu ulianza na mkutano wa Istanbul mwezi Aprili 2025, unatarajiwa kushika kasi, na huenda kasi hii ikadhihirika baada ya mkutano wa pili kati ya nchi hizo mbili, ambapo Ukraine inaweza kujiunga kwa lengo la kutangaza kusitisha mapigano. Kurekebisha mahusiano kunachukuliwa kuwa hitaji la dharura kwa Amerika kufungua mazungumzo katika faili zengine za kimkakati.

c- Mashindano ya Silaha na Nguvu za Kimkakati: Kuna uwezekano mkubwa, ikizingatiwa haja ya pande zote mbili, kwamba mazungumzo juu ya udhibiti wa silaha na nguvu za kimkakati za nyuklia na makombora yatafunguliwa haraka. Urusi huenda ikakubaliana leo na sharti la awali la Marekani kwamba China ijiunge na mazungumzo hayo, na kuyafanya kuwa ya pande tatu. Hii ni kwa sababu mikataba ya awali ya Urusi na Marekani ilikuwa ni mwendelezo wa makubaliano ya miongo kadhaa kati ya dola hizo kubwa za kijeshi, ambayo Marekani iliyakata kwa sababu ilitaka kujumuisha gwiji huyo wa China katika safu zake. Hasa kwa vile China hivi sasa inatekeleza mipango ya silaha za nyuklia ambayo hivi karibuni itaiweka kati ya safu za maagwiji hao mawili. Mpango wake wa nyuklia unatarajiwa kumiliki takriban makombora 1,000 ya nyuklia ifikapo mwaka wa 2030, ikimaanisha kuwa umepita dola za nyuklia za wastani kama vile Uingereza na Ufaransa kwa miaka. Kwa hivyo, kuna uwezekano kwamba sababu zote za kufedheheshwa kwa Urusi kuhusu kualika China kushiriki katika mazungumzo ya Urusi na Amerika juu ya silaha za kimkakati zimeondolewa. Hii inawakilisha hatua kwa Amerika katika njia yake ya kuvunja muungano wa Urusi na China. Kwa haya yote, kuna uwezekano kwamba matumaini ya Amerika ya kuvunja muungano wa Urusi na China yana uwezekano mkubwa, lakini bila kuyagonga moja kwa moja na kuumiza hisia za Urusi. Badala yake, itachukua hatua kufikia maelewano na Urusi ili kudhoofisha hatua kwa hatua muungano wa Urusi na China.

10- Hatimaye, inatia uchungu kwamba nchi za makafiri zinadhibiti dunia, na viongozi wao kukutana, kujadiliana na kupanga. Ilhali Ummah wa Kiislamu ndio Ummah bora kabisa ulioletwa kwa ajili ya wanadamu umekaa na hauna athari kwa matukio ya kimataifa. Hakika, hauna hata uwezo wa kudhibiti juu ya mambo yake yenyewe, bali yanasimamiwa na wakoloni makafiri!

Tatizo ni kwamba Ummah huu, ambao unakaribia kufikia bilioni mbili, ni mwili usio na kichwa. Dola ya Khilafah inayouunganisha haijasimamisha, na Khalifa anayesimamia mambo yake, anaye watu hupigana nyuma yake na kulindwa naye, hayupo! Hata hivyo, Khilafah itaregea, Mwenyezi Mungu akipenda, kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu (swt) na bishara njema ya Mtume wake (saw). Hata hivyo, sheria ya Mwenyezi Mungu haiwataki Malaika wasishuke kutoka mbinguni kutusimamishia Khilafah wakati Umma umekaa na haufanyi kazi ya kuisimamisha. Bali Mwenyezi Mungu hutuma Malaika kutusaidia tunapofanya kazi. Hizb ut Tahrir, kiongozi asiyewadanganya watu wake, inaulingania Ummah kufanya kazi nayo kuisimamisha (Khilafah). Hapo Uislamu na Waislamu wataheshimiwa, na ukafiri na makafiri watadhalilishwa.

[وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللَّهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ]

“Na siku hiyo Waumini watafurahi * Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.” [Ar-Rum: 4-5]

25 Safar 1447 H

19 Agosti 2025 M

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.