- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Jibu la Swali
Uvamizi wa Umbile la Kiyahudi dhidi ya Iran na Athari zake
(Imetafsiriwa)
Swali:
Al Arabiya ilichapisha kwenye tovuti yake mnamo tarehe 27/6/2025: "Vyanzo vinne vyenye taaarifa vilisema kuwa utawala wa Rais Donald Trump ulijadili uwezekano wa kuisaidia Iran kufikia hadi dolari bilioni 30 ili kujenga mpango wa nyuklia kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya kiraia. Vyanzo hivyo viliongeza kuwa majadiliano haya yaliendelea wiki hii baada ya kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano. Maafisa wa utawala wa Trump walithibitisha kwamba mapendekezo kadhaa yamewsilishwa, ya awali pamoja na yaliyoboreshwa, yakiwa na kifungu kimoja kisichobadilika, kisichoweza kujadiliwa : “kukomeshwa kabisa kwa urutubishaji wa urania ya Iran.”
Trump alikuwa ametangaza kutekelezwa kwa usitishaji vita aliopendekeza kati ya Iran na umbile la Kiyahudi. (“Netanyahu alisema amekubaliana na pendekezo la Trump. Shirika la habari la Reuters pia lilimnukuu afisa mmoja mkuu wa Iran akisema kwamba Tehran imekubali kusitishwa kwa mapigano, iliyopatanishwa na Qatar na kwa kuzingatia pendekezo la Marekani.” (Al Jazeera, 24/6/2025)
Haya yote yalitokea baada ya vikosi vya Trump kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran mnamo 22/6/2025, na baada ya umbile la Kiyahudi kuanzisha shambulizi la kushtukiza, shambulizi kubwa dhidi ya Iran mnamo 13/6/2025. Swali ni: Kwa nini umbile la Kiyahudi lilifanya uvamizi huu wa kushtukiza, wakati inatekeleza tu kwa amri ya Amerika? Pia, je si Iran inazunguka katika duara la Amerika? Kwa hivyo kwa nini Amerika ilishiriki katika kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran? Shukran.
Jibu:
Kwa jibu wazi, tutapitia mambo yafuatayo:
1- Ndio, mpango wa nyuklia wa Iran unachukuliwa kuwa tishio kubwa kwa umbile la Kiyahudi, na kwa hivyo inataka kuuondoa kwa njia zote. Kwa sababu hii, ilipongeza kujiondoa kwa Rais Trump kutoka kwa makubaliano ya 2015 mnamo 2018. Msimamo wa umbile la Kiyahudi ulikuwa wazi: linakubali tu mfano wa Libya na kuvunja kwa Iran mpango wake wa nyuklia, yaani Iran kuacha kabisa mpango wake wa nyuklia. Lilizidisha majasusi wake ndani ya Iran kwa ajili hiyo. Katika siku yake ya kwanza, shambulizi la umbile la Kiyahudi lilifichua jeshi la mawakala ndani ya Iran ambao hufuatilia na kushirikiana na shirika la kijasusi la umbile ya Kiyahudi, Mossad, kwa thamani ndogo. Wanaagiza vipuri vya droni, kuviunganisha katika karakana ndogo ndogo ndani ya Iran, na kuzirusha kwenye maeneo lengwa, ikiwa ni pamoja na nyumba za viongozi wa serikali ya Iran. Hali hii ni sawa na kile kilichotokea kwa Hezbollah nchini Lebanon wakati umbile la Kiyahudi lilipowaua viongozi wake!
2- Msimamo wa Marekani ilikuwa ndio muungaji mkono mkuu wa umbile la Kiyahudi, na kwa hakika nguvu iliyowasukuma dhidi ya mradi wa nyuklia wa Iran. Hata hivyo, Trump ameweka mezani kufanikisha hili: suluhisho la mazungumzo na suluhisho la kijeshi. Kwa hivyo, mnamo Aprili 2025, Amerika na Iran zilielekea Muscat, Oman, kwa mazungumzo. Utawala wa Trump uliwasifu kwa kina cha makubaliano yaliyofanywa katika mazungumzo ya nyuklia, kana kwamba makubaliano mapya ya nyuklia yamekaribia. Trump alikuwa ameweka makataa ya miezi miwili kukamilisha makubaliano haya. Maafisa wa umbile la Kiyahudi walikutana na mjumbe wa Marekani katika eneo na mpatanishi wa kwanza wa Iran, Witkoff, karibu mara moja kabla ya kila mkutano na wajumbe wa Iran, ili mjumbe huyo wa Marekani aweze kuwafahamisha juu ya kile kinachoendelea katika mazungumzo hayo.
3- Utawala wa Trump umetabanni mitazamo mikali ya baadhi ya viongozi wake, mtazamo ambao unaendana na umbile la Kiyahudi. Hii ilisadifiana na kuibuka kwa mitazamo mikali barani Ulaya pia. Nchi za Ulaya zilikerwa kuwa Marekani inafanya mazungumzo na Iran kipeke yake, ikimaanisha kwamba Marekani ingepokea hisa kubwa ya makubaliano yoyote na Iran, hasa kwa vile Iran ilikuwa ikiuvutia utawala wa Trump kwa mazungumzo ya mamia ya mabilioni ya dolari ambazo makampuni ya Marekani yangeweza kuwekeza na kufaidika kutoka ndani ya Iran, kama vile kandarasi za mafuta na gesi, makampuni ya ndege, na mengi zaidi. Mitazamo hii yenye misimamo mikali ilifikia kilele cha ripoti kali ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) iliyotangazwa leo, Alhamisi, Juni 12, 2025, kwamba Iran imekiuka wajibu wake katika uwanja wa kutoeneza silaha za nyuklia: "Shirika la Umoja wa Mataifa la uangalizi wa silaha za nyuklia IAEA limeishutumu Iran kwa kukiuka vikwazo vyake vya kutoeneza silaha za nyuklia kwa mara ya kwanza kwa takriban miongo miwili, duru za kidiplomasia zilisema,” (Deutsche Welle, 12/6/2025). Kiongozi Mkuu wa Iran hapo awali alikataa kusitisha urutubishaji: (Khamenei alisema: “Kwa kuwa mazungumzo yamekuja, nataka kutoa onyo kwa upande unaopinga. Upande wa Marekani ambao unashiriki katika mazungumzo haya ya moja kwa moja na kuwa na majadiliano, unapaswa kujaribu kutoeneza upuuzi ... Kusema mambo kama 'hatutaruhusu Iran kurutubisha urania’ hakuna nafasi. Hakuna mtu anayesubiri ruhusa ya mtu yeyote. Jamhuri ya Kiislamu ina sera, mwelekeo wake yenyewe, na itaendelea kuufuata.” Witkoff, mjumbe wa Trump katika Mashariki ya Kati, alisema mnamo Jumapili kwamba Washington haitakubali kiwango chochote cha kurutubisha urania katika makubaliano yanayoweza kutokea na Tehran. “Hatuwezi kuruhusu hata asilimia 1 ya uwezo wa kurutubisha,” Steven Witkoff aliiambia ABC News. “Kila kitu kinaanza kutoka kwa mtazamo wetu kwa mkataba usiojumuisha urutubishaji...” (Iran International, 20/5/2025).
4- Kwa kukataa kwa Iran kusitisha urutubishaji na msisitizo wa Amerika wa kusitisha, mazungumzo ya Amerika na Iran yalifikia mwisho, hata kama mazungumzo hayakutangazwa kumalizika. Walakini, kwa kutolewa kwa ripoti ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki mnamo 12/6/2025, umbile la Kiyahudi liliharakisha mpango uliopangwa usiku na Amerika na kuanzisha shambulizi la kushtukiza mnamo 13/6/2025, ambapo lilipiga kituo cha nyuklia cha Iran huko Natanz, kiwanda kikubwa zaidi cha kurutubisha uranium cha Iran chenye mitambo 14,000 ya centrifuge. Pia ilifanya mfululizo wa mauaji ya viongozi wa jeshi la Iran na Walinzi wa Mapinduzi, pamoja na wanasayansi wa nyuklia, na kushambulia sehemu za kurushia makombora. Bila kujali uhalali wa umbile la Kiyahudi kwa mashambulizi yake, ambao ni kwamba Iran imeanza tena utafiti na maendeleo ya silaha za nyuklia, kulingana na Netanyahu (RT, 14/6/2025). Haya yote yanakanushwa na kauli nyingi za Iran, kwamba Iran haina mpango wa kuzalisha silaha zozote za nyuklia, na kwamba inakubali kiwango chochote cha ufuatiliaji wa kimataifa ili kuhakikisha hali ya amani ya mpango wake wa nyuklia. Lakini pia ni hakika kwamba umbile la Kiyahudi lilikuwa likingojea ruhusa ya Marekani kutekeleza hilo, na pindi umbile hilo lilipoona kwamba dirisha hili lilikuwa limefunguliwa kwa idhini, lilianza mashambulizi.
5- Kwa hivyo, hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kufikiria kuwa umbile la Kiyahudi lingefanya shambulizi kama hilo bila ya idhini kutoka Amerika. Hili haliwezekani kabisa. (Balozi wa Marekani nchini ‘Israel’, Mike Huckabee, alisema mnamo Alhamisi, “Israel haiwezi kushambulia Iran bila ruhusa kutoka Washington.” (Arab48, 12/6/2025). Na baada ya mazungumzo ya simu ya dakika 40 kati ya Trump na Netanyahu, “Afisa mmoja wa Israel alilifichulia gazeti la ‘The Times’ la Israel mnamo Ijumaa kwamba Tel Aviv na Washington zilikuwa zimetekeleza ‘kampeni ya upotoshaji ya pande nyingi’ kwa ushiriki changamfu wa Donald Trump, kwa lengo la kushawishi Iran kwamba shambulizi la vifaa vyake vya nyuklia halikuwa karibu. Alieleza kuwa vyombo vya habari vya ‘Israel’ katika kipindi hicho zilikuwa zimepokea mivujo ya habari zenye kudai kuwa Trump na Netanyahu wako dhidi ya kushambulia Iran, na kuitaja mivujo hiyo “kama sehemu ya operesheni ya kuhadaa” (Al Jazeera Net, 13/6/2025). Kuongezea yote haya, Amerika ililipa umbile la Kiyahudi silaha maalum kabla ya shambulizi hilo, ambazo zilitumiwa katika shambulizi hilo: (Ripoti za vyombo vya habari zilifichua kwamba Marekani ilisafirisha kwa siri takriban makombora 300 ya maangamizi aina ya AGM-114 hadi Israel mnamo Jumanne iliyopita, kulingana na maafisa wa Marekani. Kwa mujibu wa gazeti la ‘Jerusalem Post’, “maafisa wawili wa Marekani walithibitisha kwamba Washington ilikuwa na ufahamu wa mapema wa mpango wa Jerusalem wa kushambulia shabaha za nyuklia na kijeshi za Iran mapema Ijumaa. Maafisa hao hao walisema zana za kushambulia angani kutoka ardhini za Marekani baadaye ziliisaidia Israel kupangua zaidi ya makombora ya balistiki 150 ya Iran yaliyorushwa kwa kujibu. Afisa mmoja mkuu wa ulinzi wa Marekani alinukuliwa akisema kwamba makombora ya Maangamizi “yalikuwa na manufaa kwa Israeli,” akibainisha kuwa IAF (Jeshi la Anga la Israel) lilitumia zaidi ya ndege 100 kushambulia maafisa wakuu wa Walinzi wa Mapinduzi, wanasayansi wa nyuklia na vituo vya udhibiti karibu na Isfahan na Tehran.” (Jerusalem Post; RT, 14/6/2025).
6- Kwa hivyo, utawala wa Trump uliipotosha Iran - wakati ikifanya mazungumzo nayo - kulifanya shambulizi la umbile la Kiyahudi liwe na athari kubwa kwa mshtuko na vitisho. Kauli za Marekani zinaonyesha hili, kwamba Marekani ilitaka shambulizi la umbile la Kiyahudi liwe kichocheo kwa Iran kufanya maafikiano katika mazungumzo ya nyuklia. Hii ina maana kwamba shambulizi hilo lilikuwa ala ya mazungumzo ya Marekani. Hii ni pamoja na utetezi wa umma wa Marekani wa mashambulizi ya umbile la Kiyahudi na kwamba ilikuwa ni kujilinda, na usambazaji wa silaha kwa umbile hilo na uendeshaji wa ndege za Marekani na ulinzi wa anga ili kuzima majibu ya Iran. Yote haya ni sawa na shambulizi nusu la moja kwa moja la Amerika. Miongoni mwa kauli hizi za Marekani ni kauli ya Trump, wakati wa taarifa zake kwa waandishi wa habari mnamo Jumapili, wakati akielekea kwenye mkutano wa kilele wa G7 nchini Canada, kwamba, “Wakati mwingine wanapaswa kupigana.” “Katika mahojiano na ABC, Trump alionyesha uwezekano wa Marekani kuingilia kati kuunga mkono 'Israel' katika kuondoa mpango wa nyuklia wa Iran.” (Arab48, 16/6/2025).
7- Amerika inatumia vita kama chombo cha kuitiisha Iran, kama katika taarifa ya awali ya Trump kwamba “Wakati mwingine wanapaswa kupigana, lakini wacha tutaona.” Hili linathibitishwa na maelezo ya Trump kuhusu shambulizi hili akisema, “Shambulizi la Israel dhidi ya Iran lilikuwa bora.” Alisema, “Tuliwapa nafasi na hawakuichukua. Walipigwa kwa nguvu, sana sana. Walipigwa sana kipigo cha mbwa. Na kuna mengi zaidi yanakuja, mengi zaidi.” (ABC, 13/6/2025). Trump alisema, “Wairani wanataka kujadiliana, lakini walipaswa kufanya hivyo hapo awali. Nilikuwa na siku 60, walikuwa na siku 60, na siku ya 61, nilisema, ‘Hatuna mkataba.’” (CNN, 16/6/2025). Kauli hizi zinaonyesha wazi kwamba Amerika ndiyo iliyoruhusu umbile la Kiyahudi kuanzisha uvamizi huu, na hata kuliagiza kufanya hivyo. Trump aliandika kwenye Jukwaa la Kijamii la ‘Truth’: “Iran ilipaswa kutia saini ‘mkataba’ niliowaambia watie saini... Kwa ufupi, IRAN KAMWE HAIWEZI KUWA NA SILAHA ZA NYUKLIA. Nimesema tena na tena!” (RT, 16/6/2025). Afisa mmoja wa umbile la Kiyahudi alifafanua kuhusu ushiriki wa Marekani katika ulipuaji wa mabomu ya chini chini, kwenye eneo lililoimarishwa la Fordow nchini Iran: “Marekani huenda ikajiunga na operesheni ya kijeshi dhidi ya Iran, ikibainisha kuwa Trump alisema wakati wa mazungumzo na Waziri Mkuu wa 'Israel' Benjamin Netanyahu kwamba atafanya hivyo ikiwa italazimika.” (Al Arabiya,15/6/2025).
8- Na hiki ndicho kilichotokea. Mapema Jumapili asubuhi, mnamo tarehe 22/6/2025, Trump alitangaza “kulengwa kwa vituo vitatu vya nyuklia vya Iran, kuthibitisha kufaulu kwa shambulizi la Marekani. Trump aliashiria kulengwa kwa maeneo ya nyuklia ya Fordow, Natanz, na Isfahan, akitoa wito kwa Iran kuleta amani na kukomesha vita. Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth alithibitisha kwamba shambulizi la Marekani “limeangamiza” matarajio ya kinyuklia ya Tehran.” (BBC, 22/6/2025). Kisha, CNN ilifichua Jumatatu jioni kwamba Iran ilishambulia kambi ya Marekani ya Al-Udeid nchini Qatar kwa makombora ya masafa mafupi na ya kati, ikionyesha kwamba ndege za kijeshi za Marekani zilizokuwa kwenye kambi hiyo ya anga zilihamishwa mwishoni mwa wiki iliyopita. Shirika la habari la Reuters pia liliripoti: “Iran ilitoa taarifa mapema kwa Marekani kupitia njia za kidiplomasia saa chache kabla ya shambulizi hilo, pamoja na mamlaka za Qatar.” (Sky News Arabia, 23/6/2025). Mnamo Jumatatu, Trump alisema, “Ninataka kuishukuru Iran kwa kutupa taarifa ya mapema ... ambayo iliwezesha kutopotea kwa maisha ya watu, na kutojeruhiwa mtu yeyote.” (Sky News, 24/6/2025).
9- Kisha, baada ya mashambulizi haya ya Marekani na umbile la Kiyahudi na majibu ya Iran, ambapo hasara ya mali ilikuwa kubwa pamoja na hasara ya binadamu: “Msemaji wa Wizara ya Afya ya Iran alisema kwamba mashambulizi ya Israel yalisababisha mauaji ya watu 610 na kujeruhiwa kwa wengine 4,746 tangu mwanzo wa mzozo ... Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ... kiwango cha vifo tangu Juni 13 kimeongezeka hadi watu 28 ...” (Habari za BBC, 25/6/2025), baada ya mashambulizi haya, Trump, kama alivyoyaanzisha kwa kulisukuma umbile la Kiyahudi kuishambulia Iran na kushiriki katika hilo, sasa anatangaza usitishaji vita, ili Mayahudi na Iran wakubaliane, kana kwamba Trump ndiye anayesimamia vita kati ya pande mbili na pia ndiye anayesimamisha vita! “Trump alitangaza kutekelezwa kwa usitishaji vita aliopendekeza kati ya Iran na umbile la Kiyahudi.” “Netanyahu alisema kwamba alikubaliana na pendekezo la Trump. Shirika la habari la Reuters pia lilimnukuu afisa mkuu mmoja wa Iran akisema kwamba Tehran ilikubali kusitisha mapigano kwa upatanishi wa Qatar na pendekezo la Marekani.” (Al Jazeera, 24/6/2025). Hii ina maana kwamba vita hivi ambavyo Trump alivianzisha na kisha kuvisimamisha vilikuwa ni kufikia lengo lake la kuondoa ufanisi wa silaha za nyuklia na makombora ya Iran (katika taarifa yake kwa waandishi wa habari kabla ya kuondoka kuhudhuria mkutano wa NATO jijini The Hague, Trump alisema, “Maeneo ya nyuklia ya Iran yameangamizwa kabisa!” na kamwe haitajenga upya mpango wake wa nyuklia.” Aliendelea kusema, “Israel haitaishambulia Iran... na usitishaji vita umeanza kutekelezwa.” (Al Jazeera, 24/6/2025).
10- Ama kuhusu Iran kuzunguka katika duara la Amerika, ndio, Iran ni dola inayozunguka katika duara la Amerika, inataka kufikia maslahi yake kwa kufikia maslahi ya Amerika. Kwa hivyo, iliisaidia Amerika kuzikalia kimabavu Afghanistan na Iraq na kuimarisha uvamizi wake huko. Pia iliingilia kati nchini Syria ili kumlinda kibaraka wa Amerika, Bashar al-Assad, na ilifanya vivyo hivyo nchini Yemen na Lebanon. Kwa kufanya hivyo, inatafuta kufikia maslahi yake katika nchi hizi na kuwa dola kuu ya kikanda katika eneo hilo, hata kama inazunguka katika duara la Amerika! Hata hivyo, walisahau kwamba wakati Amerika inapoona kwamba maslahi yake yamekwishia katika dola inayozunguka duara lake na inataka kupunguza dori yake na mamlaka yake, huishinikiza kidiplomasia, na ikiwa ni lazima, kijeshi, kama inavyotokea kwa Iran katika mashambulizi ya hivi karibuni, ili kudhibiti kasi ya dola inayozunguka katika mzunguko wake. Kwa hiyo, kupitia shambulizi hili lililoamriwa na kutekelezwa na umbile la Kiyahudi na kwa uungaji mkono wake, linaumaliza uongozi wa kijeshi, hususan kitengo cha nyuklia na washauri ambao hivi karibuni wamejaribu kuwa na sauti katika kukabiliana na umbile la Kiyahudi dhidi ya matakwa ya Marekani. Haijali kuhusu nchi hizi kwa sababu inatambua kwamba nchi hizi hatimaye zitakubali suluhisho lililoundwa na Amerika!
11- Hili ndilo lililoanza kuonekana hadharani katika mpango wa Marekani baada ya kusitishwa kwa mapigano, ambayo ni kukomesha silaha za nyuklia za kijeshi za Iran: (Vyanzo vinne vilivyo na taarifa vilisema kuwa utawala wa Rais Donald Trump ulijadili uwezekano wa kuisaidia Iran kufikia hadi dolari bilioni 30 kujenga mpango wa nyuklia kwa ajili ya kuzalisha nishati kwa madhumuni ya kiraia, kupunguza vikwazo na kupunguza mabilioni ya dolari kwa kiasi kikubwa cha fedha za Iran zilizozuiliwa, ambayo yote haya ni sehemu ya jaribio kali la kuirudisha Tehran kwenye meza ya mazungumzo, kwa mujibu wa mtandao wa habari wa CNN ya Amerika. Vyanzo hivyo vya habari viliripoti kuwa wahusika wakuu kutoka Marekani na Mashariki ya Kati walifanya mazungumzo na Wairani nyuma ya pazia, hata katikati mwa wimbi la mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran na Israel katika kipindi cha wiki mbili zilizopita. Vyanzo hivyo viliongeza. Majadiliano haya yaliendelea wiki hii baada ya makubaliano ya kusitisha vita kufikiwa. Maafisa wa utawala wa Trump walithibitisha mapendekezo kadhaa yaliwasilishwa, ya awali na yaliyoboreshwa, yenye nukta moja isiyobadilika, isiyoweza kujadiliwa: “kusitishwa kikamilifu kwa urutubishaji wa urania ya Iran.” (Al Arabiya, 27/6/2025)
12- Hatimaye, janga la Ummah huu liko kwa watawala wake. Iran ilitishiwa kushambuliwa, lakini haikuanzisha mashambulizi ya kujilinda, ingawa shambulizi ndio njia bora ya kujilinda dhidi ya Mayahudi. Badala yake, ilikaa kimya hadi vifaa vyake vikapigwa na wanasayansi wake kuuawa, na kisha kuanza kujibu. Vile vile hili linatekelezeka kwa shambulizi la Amerika. Kisha Trump akatangaza kusitisha mapigano, na Mayahudi na Iran wakakubali. Baada ya hapo, Amerika ilifanya mijadala na kutoa mapendekezo, na kusema kwamba “kusitishwa kabisa kwa urutubishaji wa urania ya Iran” ni jambo la kudumu na haliwezi kujadiliwa! Tunaonya kwamba vita hivi vinaweza kupelekea aina yoyote ya “mpango wa amani” na umbile la Kiyahudi, au kupokonywa silaha kwa Iran. Ama kuhusu watawala wengine katika nchi za Waislamu, hasa walio karibu na umbile la Kiyahudi, ndege za adui zinaruka juu ya vichwa vyao, na kuzipiga mabomu nchi za Kiislamu, na kisha kurudi zikiwa zikiwa salama bila hata kufyatuliwa risasi moja kwao!! Wako mikononi mwa Amerika... wanahalalisha kutulia tuli, wanaitukuza mipaka, na wanasahau au wanajifanya kusahau kuwa ardhi za Waislamu ni moja, iwe iko mbali zaidi duniani au karibu zaidi! Na kwamba amani ya Waumini ni moja, na vita vyao ni vimoja, si sawa kwa madhehebu yao kuwagawanya maadamu wao ni Waislamu... Watawala hawa wameangamia, kwani wanadhani kwamba kwa utiifu huu kwa Marekani wataokolewa, na hawatambui kwamba Marekani itawatenga na kuwapokonya silaha, endapo watakuwa tishio kwa umbile la Mayahudi, kama ilivyofanya nchini Syria iliporuhusu umbile la Kiyahudi kuangamiza zana za jeshi la Syria na sasa inafanya vivyo hivyo nchini Iran. Watawala hawa watarithi udhalifu duniani na Akhera:
[سَيُصِيبُ الَّذِينَ أَجْرَمُوا صَغَارٌ عِنْدَ اللهِ وَعَذَابٌ شَدِيدٌ بِمَا كَانُوا يَمْكُرُونَ]
“Itawafikia hao walio kosa udhalili na adhabu kali kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya vitimbi walivyo kuwa wakivifanya.” [Al-An’am: 124]. Je, wataelewa? Au wao ni:
[صُمٌّ بُكْمٌ عُمْيٌ فَهُمْ لَا يَعْقِلُونَ]
“… viziwi, mabubu, vipofu, kwa hivyo hawaelewi.” [Al-Baqara: 171].
Enyi Waislamu: Mnaona na mnasikia yale ambayo watawala wenu wamewaleteeni ya udhalilifu, fedheha, na kuwanyenyekea makafiri wakoloni, hata Mayahudi ambao wamedhalilishwa na kuwa mafukara wanaikalia kimabavu Ardhi Iliyobarikiwa! Bila shaka mnajua kwamba hamtakuwa na izza isipokuwa kwa Uislamu na dola ya Kiislamu, Khilafah Rashida, ambayo ndani yake Khalifa Muongofu anakuongozeni, ambaye nyuma yake mnapigana na mnalindwa naye, na hili litatokea, Mwenyezi Mungu Akipenda, mikononi mwa waumini wenye ikhlasi, na maneno yake (saw) yatatimia:
«لَتُقَاتِلُنَّ الْيَهُودَ فَلَتَقْتُلُنَّهُمْ...»
“Mtapigana na Mayahudi na mtawaua” Kisha ardhi itang’aa kwa ushindi wa Mwenyezi Mungu Al Qawi, Al Aziz, Al Hakeem (Mwenye Nguvu, Mwenye izza, Mwenye hekima).
Kwa kumalizia, Hizb ut Tahrir, kiongozi asiyewadanganya watu wake, inakulinganieni kuinusuru na mufanye kazi nayo kuiregesha Khilafah Rashida kwa mara nyingine tena, ili Uislamu na wafuasi wake uheshimiwe; na ukafiri na wafuasi wake udhalilike, na huo utakuwa ndio ushindi mkubwa.
[وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ]
“Na siku hiyo Waumini watafurahi * Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.” [Ar-Rum: 4-5]
3 Muharram 1447 H
28/6/2025 M